Mahakama yaamuru Alex Msama wa Tamasha la Pasaka, mwenzake wakamatwe

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu imeamuru na kutoa hati ya kukamatwa kwa mfanyabiashara, Alex Msama na mwenzake Benny Sammoh na kufikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Amri hiyo ilitolewa jana Jumatano, Januari 21, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube kufuatia maombi ya Serikali, kutokana na kuruka dhamana ya Polisi.

Msama, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Msama Promotion, mwandaaji  wa Tamasha la Pasaka na mwenzake Sammoh wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, lakini wanadaiwa kukimbia kukwepa kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka hayo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka  Msama, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Dira Media, na mwenzake Sammoh walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na baada ya kuhojiwa kwa tuhuma zinazowakabili, wakaachiwa kwa dhamana.

Hata hivyo, baadaye wamekuwa wakiitwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani bila mafanikio na wanadaiwa kuwa hawapo jijini Dar es Salaam.

Wanadaiwa baada ya kufuatiliwa mara ya mwisho walionekana Nzega Tabora na wamekuwa wakikwepa kukamatwa.

Hivyo jana Jumatano Januari 21, 2026 Jamhuri iliwafungulia kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu ambayo imepangwa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.

Baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Kafuko waliiomba mahakama itoe hati ya kuwakamata popote pale walipo na kufikishwa mahakamani hapo kukabiliana na kesi yao hiyo.

Mahakama baada ya kusikiliza ombi hilo upande mmoja imelikubali na ikatoa hati ya kuwakamata popote walipo, huku ikielekeza baada ya kuwakamata wafikishwe mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Kwa mujibu wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 1371/2026, ambayo Mwananchi limeiona nakala yake, washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka manane.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu wa kupanga, kinyume na Aya ya 4(1)(a) ya Jedwali la Kwanza pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) vyote vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, [Sura ya 200 Toleo la Marejeo ya 2023].

Wanadaiwa kuwa Juni 26, 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Dar es Salaam, kwa pamoja na kwa makusudi walipanga na kuongoza mtandao wa kihalifu, yaani kupata fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili, Sammoh peke yake anadaiwa kughushi nyaraka, kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, [Sura ya 16 Toleo la Marejeo ya 2023].

Anadaiwa kuwa Aprili 22, 2001 huko Kigamboni Vijibweni ndani ya Wilaya ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya, alighushi hati, yaani mkataba wa mauzo ya ardhi.

Mkataba huo unadaiwa kuwa unaonyesha kuwa alinunua kiwanja kutoka kwa Mwinyikondo Hela, ambacho baadaye kilipimwa na kusajiliwa kama kiwanja namba 33 chenye hati ya umiliki namba 129621 kilichopo Vijibweni Industrial Area, jambo ambalo alijua si la kweli.

Shtaka la tatu ni la kutumia nyaraka za uongo, kinyume na vifungu vya 342 na 337 vya Kanuni ya Adhabu, ambalo pia linamkabili Sammoh peke yake.

Anadaiwa kuwa Mei 30, 2018 katika Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kupotosha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Temeke katika shauri namba 128 la mwaka 2014, akiwa shahidi, kwa kujua na kwa udanganyifu alitumia nyaraka za uongo, yaani mkataba huo wa mauzo ya ardhi.

Shtaka la nne ni la kutunga ushahidi wa uongo kinyume na kifungu cha 106(b) cha Kanuni ya Adhabu, [Sura ya 16 Toleo la Marejeo ya 2023], ambalo pia linamkabili Sammoh peke yake.

Anadaiwa kuwa Mei 30, 2018 wilayani Temeke, mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya kupotosha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Temeke katika shauri namba 128 la mwaka 2014, akiwa shahidi, aliwasilisha mbele ya baraza hati ya kughushi, yaani mkataba huo wa mauzo ya ardhi.

Shtaka la tano ni la kuapa uongo, kinyume na vifungu vya 107 na 104 vya Kanuni ya Adhabu, ambalo vilevile linamkabili Sammoh peke yake.

Anadaiwa kuwa Machi 23, 2018 wilayani  Temeke, mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya kupotosha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Temeke katika mwenendo wa shauri namba 128 la 2014, akiwa shahidi, alifungua shauri hilo na akaapa kwa jina la Ben Samson badala ya jina lake halali la Benny  Mwita Sammoh.

Shtaka la sita ambalo linawahusu washtakiwa wote wawili, Sammoh na Msama ni la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kinyume na vifungu vya 301 na 302 vya Kanuni ya Adhabu, [Sura ya 16 Toleo la Marejeo ya 2023].

Wanadaiwa kuwa Juni 26, 2023 jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu na kwa nia ya kudanganya, walipata fedha kiasi cha Sh984 milioni kwa kuuza kiwanja namba 33 chenye Hati ya Umiliki Na. 129621 kilichopo Vijibweni Industrial Area, mali ya kampuni ya World Oil (Tanzania) Ltd.

Wanadaiwa kuwa waliuza kiwanja hicho kwa madai ya uongo kwamba mshtakiwa wa kwanza Sammoh ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Wanadaiwa kuwa walidai kuwa Sammoh ndiye mmiliki kwa mujibu wa hukumu ya shauri la madai namba 128 la 2014 la Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Temeke na Rufaa namba 120 ya mwaka 2014 katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Dar es Salaam.

Hivyo wanadaiwa kiwa walijipatia fedha hizo ilhali wakijua kuwa hukumu hizo zilipatikana kwa kutumia mkataba wa mauzo ya ardhi wa kughushi na ushahidi wa uongo.

Shtaka la saba ni la utakatishaji fedha kinyume na vifungu vya 12(1)(d) na 13(1)(a) vya Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha, [Sura ya 423 Marejeo ya 2023], vikisomwa pamoja na Aya ya 22 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, [Sura ya 200 Marejeo ya 2023].

Anadaiwa katika tarehe mbalimbali kati ya mwaka 2023 na 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, alipokea na kumiliki fedha kiasi cha Sh984 milioni kupitia Akaunti ya Benki namba 011148002353 iliyo katika jina lake katika Tawi la NBC Corporate.

Anadaiwa kuwa alipokea na kumiliki fedha hizo, ilhali akijua kuwa ni mapato yatokanayo na kosa la msingi la kupata fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la nane pia ni la utakatishaji fedha kinyume na vifungu vya sheria vilivyotajwa katika shtaka la saba, ambalo linamkabili Msama. 

Anadaiwa katika tarehe mbalimbali za mwaka 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, alipokea na kumiliki fedha kiasi cha Sh370 milioni kupitia Akaunti ya Benki namba 011148002353 katika Tawi la NBC Corporate.

Anadaiwa kuwa alipokea na kumiliki fedha hizo ilhali alijua kuwa ni mapato yatokanayo na kosa la msingi la kupata fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena mahakamani hapo Februari 25, 2026.