Davos. Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema anatafakari mpango anaouita “makubaliano ya mwisho”, unaolenga kuwapa wakazi wa Greenland, ofa ya hadi dola milioni moja kwa kila mtu endapo wataidhinisha kujiunga na Marekani kupitia kura ya maoni.
Pendekezo hilo linaelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Marekani kuimarisha masilahi yake ya kiusalama na kijiografia katika eneo hilo lenye idadi ya takribani watu 57,000.
Greenland ni kisiwa kikubwa zaidi duniani kilichopo kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki na karibu na eneo la Aktiki. Licha ya jina lake kudokeza rangi ya kijani, zaidi ya asilimia 80 ya eneo la Greenland limefunikwa na barafu nene mwaka mzima, hali inayosababisha kuwa moja ya maeneo yenye baridi kali zaidi duniani.
Kisiasa, Greenland si nchi huru bali ni eneo linalojitawala chini ya Ufalme wa Denmark. Ina serikali yake ya ndani inayosimamia masuala mengi ya ndani, huku Denmark ikibaki na mamlaka ya masuala ya ulinzi na uhusiano wa kimataifa. Hata hivyo, Greenland inaendelea kuwa na umuhimu mkubwa kimkakati na kimazingira duniani, hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na rasilimali zilizopo chini ya barafu lake.
Kiasi hicho alichotoa Trump kwa wakazi wa Greenland ni sawa na takribani pauni 750,000 au euro 850,000 kwa kila mkazi.
Hata hivyo, kauli hiyo imezua mjadala mpana kimataifa kuhusu uhuru wa Greenland na nafasi ya mataifa makubwa katika siasa za kimataifa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Trump kusema wazi kuwa hatatumia nguvu kuchukua kisiwa hicho, kauli iliyopokelewa vyema na wawekezaji na kuchochea ongezeko la soko la hisa.
Pendekezo hilo limeendelea kuzua mjadala mkali kimataifa, huku Denmark ikisisitiza kuwa umiliki wa Greenland ni “mstari mwekundu” usiovukwa.
Pia, Trump ameondoa vitisho vya kutumia nguvu au kutoza ushuru dhidi ya washirika wa umoja wa kujihami wa nchi za magharibi (Nato), kufuatia mvutano ulioibuka kuhusu mustakabali wa Greenland, akidai sasa kuna mfumo wa makubaliano ya baadaye kuhusu usalama wa eneo hilo.
Akizungumza baada ya mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte, jana, Trump alisema amesitisha mipango ya kutoza ushuru kwa Uingereza na mataifa mengine yaliyopinga wazo lake la Marekani kupata udhibiti wa kisiwa hicho.
Katika hotuba yake kwenye Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos, Trump aliwakosoa washirika wa Ulaya kuhusu nishati, uhamiaji na mchango wao kwa ulinzi wa pamoja, akidai Marekani imekuwa ikibeba mzigo mkubwa bila malipo ya kutosha.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer alisema hatayumba chini ya vitisho vya ushuru wala shinikizo la kisiasa kuhusu mustakabali wa Greenland, akisisitiza msimamo wa kuheshimu uhuru na sheria za kimataifa.
Pia, alidokeza uwezekano wa kukataa kujiunga na bodi ya amani inayopendekezwa na Trump endapo itahusisha Russia.
Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wa Marekani, akiwemo Seneta Lindsey Graham, walipongeza uamuzi wa kuondoa matumizi ya nguvu, lakini wakasema hoja za kiusalama za Marekani kuhusu Greenland zinapaswa kujadiliwa ndani ya Nato.