Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwaaga vijana 228 wanaoelekea kufanya kazi nje ya nchi baada ya kupata ajira, Wakala binafsi wa ajira wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi na uzalendo.
Hiyo itasaidia kuepuka vitendo vinavyokiuka sheria, hususan kuwanyanyasa Watanzania wanaotafuta ajira ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Januari 22, 2026 na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Uhusiano), Zuhura Yunus wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 228 wanaoelekea kufanya kazi katika nchi mbalimbali.
Aidha, Zuhura amewahimiza vijana wote wanaosaka ajira nje ya nchi, wafuate utaratibu sahihi ikiwemo kutumia mawakala waliosajiliwa kisheria na kuhudhuria mafunzo maalumu kabla ya kusafiri.
Amesema hilo litawasaidia kuepuka kutumia njia zisizo rasmi zinazoweza kuwaweka hatarini.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa mawakala binafsi wa ajira wanaojishughulisha na uunganishaji wa Watanzania kupata ajira ndani na nje ya nchi kwani umefungua kwa kiasi kikubwa fursa za ajira kwa vijana.
“Hivyo, fanyeni kazi kwa uadilifu, uwazi na uzalendo ili kuepuka vitendo vyote vinavyokiuka sheria kwa kuwanyanyasa Watanzania wanaotafuta ajira ndani na nje ya nchi,” amesema Zuhura.
Ameongeza kuwa mawakala wanapaswa kuzingatia masilahi ya wafanyakazi kabla ya kutanguliza faida kwa kuwapatia taarifa sahihi, mikataba halali, mazingira salama ya kazi na kuwahakikishia ulinzi wa haki zao wanapokuwa nje ya nchi.
Zuhura amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayokiuka utaratibu akisema lengo ni kulinda usalama, utu na haki za Mtanzania popote alipo.
Kwa mujibu wa Zuhura, kuanzia Novemba 2025 hadi Januari 2026, jumla ya vijana 1,638 wameunganishwa na ajira nje ya nchi, zikiwamo Saudi Arabia, Qatar, Oman na Ujerumani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Omary Mziya amewataka vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa nchi kwa kufanya kazi kwa weledi, kujali muda na kuzingatia maadili ya kazi, hatua itakayoliletea Taifa sifa njema.
“Mnapokuwa huko msisahau nyumbani. Jengeni uchumi wa nchi kwa kuweka akiba; Mfuko wa NSSF unaendelea kutoa huduma hata mkiwa nje ya nchi, jambo litakalowasaidia baadaye wakati wa uzeeni,” amesema Mziya.
Naye Mwenyekiti wa Mawakala wa Ajira nchini, Abdallah Mohamed amesema awali mawakala wa ajira walikumbana na changamoto nyingi katika utendaji wao, lakini kwa juhudi za Serikali, mazingira ya kazi yameboreshwa na kuwezesha utendaji bora zaidi.
“Vijana mnaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, ninyi ni nguzo ya Taifa. Msiende mkaifedhehesha Serikali ya Tanzania,” amesema Mohamed.