Zanzibar yazindua kampeni ya “Visit Zanzibar” jijini London

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Zanzibar imezindua rasmi kampeni yake ya kwanza kabisa ya masoko ya utalii ya kimataifa ijulikanayo kama Visit Zanzibar jijini London, Uingereza, ikitumia mabasi maarufu ya kisasa ya jiji hilo.

Zinduzi huo  ni jukwaa lenye mvuto mkubwa la kutangaza visiwa hivyo kwa mamilioni ya wakazi na wageni wa kimataifa wanaotembelea London.

Kampeni hiyo imezinduliwa na Balozi wa Tanzania nchini  Uingereza na Jamhuri ya Ireland, Mbelwa Kairuki, na ni mpango wa kimkakati wa Tume ya Utalii Zanzibar (ZCT).

Lengo la kampeni hiyo ni kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu Zanzibar kama kivutio cha utalii na kuchochea ongezeko la idadi ya watalii wanaoingia visiwani humo.

Kampeni hii ya kihistoria ya kimataifa inatekelezwa kama matokeo ya moja kwa moja ya ziara yenye mafanikio iliyofanywa London na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, mwezi Aprili 2025, ambapo kuimarisha ushirikiano na kupanua uwepo wa Zanzibar katika soko la utalii duniani ilikuwa miongoni mwa vipaumbele.

Mabasi ya London kuonesha Zanzibar kwenye njia za katikati ya jiji

Kama sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo, mabasi yaliyopakwa nembo ya Visit Zanzibar yanaondoka katika Kituo cha Shepherd’s Bush Depot na kuanza kufanya kazi kwenye njia mbalimbali zenye msongamano mkubwa katikati ya jiji la London.

Hatua hiyo inalenga wakazi wa London pamoja na takribani wageni wa kimataifa milioni 20 waliotembelea jiji hilo mwaka 2024, kwa mujibu wa londonandpartners.com.

Basi lenye nembo ya Visit Zanzibar linafanya kazi kwenye Njia ya 94, mojawapo ya njia zinazoonekana zaidi katika maeneo ya katikati ya London, likipita katika maeneo muhimu ya utalii, burudani na biashara kama Piccadilly Circus, Regent Street, Oxford Street na Marble Arch, kisha kuendelea magharibi kupitia Shepherd’s Bush hadi Acton.

Mpangilio huo unahakikisha simulizi ya Zanzibar katikati ya jiji, na kuwafikia wasafiri wa kila siku, wakazi na wageni wanaotembelea London.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Balozi Kairuki alisema London ni miongoni mwa miji inayotembelewa zaidi duniani, ikipokea zaidi ya wageni wa kimataifa milioni 20 kila mwaka, na kuwa lango kuu la dunia linalounganisha Ulaya, Amerika Kaskazini, Mashariki ya Kati na Afrika.

“Kwa Zanzibar, hilo linaifanya London kuwa jukwaa bora kabisa la kuonesha visiwa vyetu kwa hadhira ya kweli ya kimataifa. Basi la London lenye hadhi ya kipekee husafiri katikati ya jiji na kupita mbele ya mamilioni ya wakazi, abiria na wageni kila siku, hivyo kuwa mojawapo ya njia zenye nguvu na zinazoonekana zaidi za matangazo ya utalii,” alisema Balozi Kairuki.

Alieleza kuwa uzinduzi huo ni wa kipekee kwa sababu ni mara ya kwanza Zanzibar kutekeleza kampeni maalumu ya matangazo ya nje jijini London.

Kupitia mpango huu, alisema Zanzibar inajivunia kuitambulisha kwa hadhira mpya kama kivutio cha kiwango cha juu chenye utamaduni, historia na mapumziko ya hali ya hewa ya joto, pamoja na kuimarisha ushirikiano unaokua wa utalii kati ya Zanzibar, Tanzania na Uingereza.

Mpango wa kimkakati wa Tume ya Utalii Zanzibar

Kampeni hiyo inaongozwa na Tume ya Utalii Zanzibar kama sehemu ya mkakati wake wa masoko ya kimataifa na kujenga chapa ya Zanzibar.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Utalii Zanzibar, Bw Arif Abbas Manji, alisisitiza umuhimu wa mpango huo, akisema Tume inaamini huu ni mpango wa kihistoria wa kuitangaza Zanzibar ambao haupaswi kukosa.

Alisema ni fursa muhimu ya kuinua hadhi ya Zanzibar kimataifa na kuvutia watalii wengi zaidi kwa manufaa makubwa ya kiuchumi.

Kufungua soko lenye thamani kubwa

Uingereza bado ni moja ya masoko muhimu ya utalii kwa Zanzibar.

Hadhi ya London kama kitovu kikubwa cha kimataifa inamaanisha kampeni hii itafikia hadhira pana kutoka mataifa mbalimbali kila siku na kuwahamasisha wasafiri kugundua utamaduni, urithi, fukwe na ukarimu wa Zanzibar.

Kwa kuunganisha chombo maarufu duniani cha matangazo ya nje pamoja na jiji linalovutia mamilioni ya wageni wa kimataifa, Zanzibar inalenga kuimarisha uhusiano na soko la Uingereza, kupanua uelewa wa safari za masafa marefu, na kuchochea ongezeko la watalii na uwekezaji katika sekta ya utalii ya visiwa hivyo.