Dk Mwigulu atoa maagizo mapya utatuzi wa kero za wananchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuhamia kwa ofisi zote za umma katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma kunapaswa kurahisisha utoaji wa huduma na kushughulikia kero za wananchi kwa haraka na ufanisi.

Amesema badala ya kuandikiana barua zinazoongeza urasimu, watumishi wa umma wanapaswa kukutana ana kwa ana ili kutatua changamoto zinazohusu wananchi na miradi ya maendeleo, kwani ofisi zote zipo karibu katika eneo moja.

Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi, Januari 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kawaida ya kukagua Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, ambapo pia amekagua jengo la makao makuu ya Wizara ya Maji lililojengwa kwa gharama ya Sh22.9 bilioni.

“Tunaendelea kusisitiza matumizi ya sanduku la posta, lakini ofisi zote za umma zipo hapa Mtumba. Linapokuja suala linalohusu Watanzania au miradi ya maendeleo, linahitaji utatuzi wa haraka hatuna sababu ya kuandikiana barua wakati ofisi zetu zipo karibu,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema haridhishwi na taarifa za utekelezaji zinazojikita katika kunukuu barua zilizotumwa au kupokewa, badala ya uamuzi wa vitendo uliofikiwa kwa kukutana na kujadiliana ana kwa ana.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maji alipotembelea Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, Januari 22, 2026. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi, wa pili kulia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu



“Nimekuwa nikiona kwenye vikao taarifa za utekelezaji zinaelezwa kwa kusema barua ilishapelekwa wizara fulani. Unaandikaje barua wakati ofisi zinatazamana? Kama mnataka kumbukumbu, andikeni muhtasari wa kikao,” amesisitiza.

Amesema barua ni nusu ya kuonana, na haiingii akilini kuona watumishi wa ofisi zilizo jirani wakitumia miezi kusubiri majibu ya barua kupitia posta.

“Tunaandika barua, miezi inapita, tena mnatumia Posta. Hayo yalikuwa ya zamani. Kama tunahitaji kumbukumbu, tuandike taarifa ya kikao iliyoainisha kilichokwama, waliokutana na makubaliano yaliyofikiwa, kisha utekelezaji uanze,” amesema.

Kukazia suala hilo, Dk Mwigulu ametoa maelekezo kwa makatibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma kutokubali taarifa za utekelezaji zinazotegemea barua pekee.

Amesema kuendekeza utamaduni huo si jambo sahihi na linapaswa kukoma huku akisema mtumishi anayeshindwa kutumia fursa ya ukaribu wa ofisi kutatua changamoto kwa haraka ni mzigo kwa Serikali.

“Nimelisema hili ili kuelekeza ofisi zote za Serikali. Tupo karibu. Katibu Mkuu ukiona mtumishi anakuletea taarifa ya utekelezaji kwa kutegemea barua, mkemee hapohapo. Akirudia, jua huyo hafai,” amesema Dk Mwigulu.

Wizara zinazosuasua kuhamia Dodoma

Serikali imezitaka wizara na taasisi za umma ambazo bado zinaendelea kufanya kazi Dar es Salaam licha ya kuwepo kwa miundombinu Dodoma, kuhamia rasmi katika Mji wa Serikali Mtumba, ili kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Serikali katika makao makuu ya nchi.

Kukazia suala hilo, Dk Mwigulu amesema amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, kumuelekeza Katibu Mkuu kuunda timu maalumu itakayofanya tathmini ya majengo yote ya taasisi za serikali yaliyopo Dar es Salaam, ambayo taasisi zake zinapaswa kuhamia Dodoma.

Watumishi wa Wizara ya Maji wakimsikiliza Waziri Muu, Dk Mwigulu Nchemba alipozungumza wakati alipotembelea makao makuu ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma, Januari 22, 2026. 



Dk Mwigulu amesema majengo hayo yatakayobainika hayatumiki tena yatagawiwa kwa taasisi nyingine za Serikali ambazo hazina wajibu wa kuhamia Dodoma, lakini zinahitaji ofisi.

“Hapa ndiyo makao makuu ya nchi. Hapa siyo kambi, na wala hatutakuwa na makao makuu mawili yanayokwenda sambamba. Taasisi ambazo ofisi zake tayari zimekamilika hapa Dodoma lakini bado zinashikilia ofisi Dar es Salaam wakati kuna taasisi nyingine zinazohitaji majengo, hali hiyo siyo sahihi,” amesema.

Amesema Serikali imehamia Dodoma kikamilifu na haiwezi kufanya kazi kwa mfumo wa mpito.

“Nitumie fursa hii kuzielekeza taasisi zote kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma. Tumehamia hapa kikamilifu, hii siyo kambi, kwa sababu ukiwa kambini unakuwa unawaza lini utarudi nyumbani,” amesema.

Muonekano wa Majengo mbalimbali yaliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.



Dk Mwigulu amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha shughuli zote muhimu za Serikali zinafanyika Dodoma ili kuwasogezea huduma Watanzania kutoka pande zote za nchi, kwa kuwa mji huo uko katikati na unarahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Waziri Lukuvi, amesema awamu ya pili ya ujenzi wa majengo 29 ya Serikali imeanza kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kati ya majengo hayo, 24 ni ya wizara mbalimbali huku matano yakihudumia taasisi za Serikali.

“Katika majengo hayo, moja lipo Kikombe karibu na Chamwino ambalo ni jengo la ulinzi. Majengo haya yote 29 yalianza katika awamu ya sita. Nakumbuka tulipoanza kuhamia Dodoma tulikuwa na majengo madogo yaliyotuwezesha kufanya kazi,” amesema Lukuvi.

Ameongeza baada ya Rais Samia kuingia madarakani, alianza utekelezaji wa ujenzi wa majengo makubwa na ya kisasa, hatua ambayo imeongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Serikali na kuimarisha makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa jengo la makao makuu ya wizara hiyo fedha haijawahi kuwa kikwazo ndiyo maana limekalika kwa wakati.

“Tumepata mkandarasi mzuri na msimamizi alikuwa mzuri na tunakuahidi Waziri Mkuu kwa jengo hili tutafanya kwazi kwa weledi usiku na mchana kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani,” amesema Aweso.