RAIS wa Bigman FC, Ahmed Waziri Gao amesema hana mpango wa kuiuza timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu kwa sasa, licha ya kudaiwa pia huenda ikapigwa bei kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gao alisema licha ya gharama kubwa za uendeshaji zinazoendelea kwa sasa, ila hana mpango kabisa wa kuiuza, japo ikiwa kuna mtu yeyote atakayetoa kiasi cha zaidi ya Sh800 milioni huenda akabadili msimamo wake.
“Mimi nimesikia tu suala la kuuzwa kama ambavyo wewe umeniuliza lakini hilo jambo halipo, binafsi nina uwezo mzuri wa kuiendesha ila kukiwa na mabadiliko mengine ya kiuendeshaji basi nakuahidi utakuwa wa kwanza kujua hilo,” alisema Gao.
Gao alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha anaendelea kuwekeza kwa nguvu katika timu hiyo kwa kusajili wachezaji bora na wenye majina makubwa, ili kutoa ushindani ambao utakiwezesha kikosi hicho kutimiza malengo ya kucheza Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kiasi cha fedha ambacho kimewekwa kwa ajili ya kuuzwa kwa timu hiyo ni Sh300 milioni, ingawa, Rais Gao anataka anayeihitaji kwa ajili ya kuinunua aweke zaidi ya Sh800 milioni ili afanye uamuzi wa mwisho.
Timu hiyo zamani iliyofahamika Mwadui FC, katika Ligi ya Championship msimu huu iko nafasi ya nane na pointi 20, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, ikitoka sare mitano na kupoteza pia mitano, huku ikifunga mabao 13 na kuruhusu 12.