Fountain Gate kuhamia Arachuga | Mwanaspoti

UONGOZI wa Fountain Gate huenda ukahamishia mechi zake zote za nyumbani zilizobaki za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, baada ya kuutumia tangu mwanzo Tanzanite kwaraa uliopo mjini Babati, Manyara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema ni kweli timu hiyo imepata mwaliko na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla kwa ajili ya kwenda kuutumia uwanja huo, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa.

“Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, ndiye aliyependekeza tukachezee Arusha na ukiangalia pia tunaendelea na maboresho katika baadhi ya maeneo ya uwanja wetu wa Tanzanite Kwaraa, japo hatujafikia uamuzi wa mwisho wa hilo,” alisema Wendo.

Wendo alisema ikiwa timu hiyo itahamishia mechi zake zote zilizobakia Arusha wataweka wazi kwa mashabiki na wadau wa kikosi hicho, japo kwa sasa uongozi unachokifanya ni kuendelea na maboresho ya kusajili pia wachezaji wengine wapya.

“Mchakato ulio mbele yetu ni kuongeza nyota wengine wapya kutokana na ripoti ya benchi la ufundi, hadi sasa kuna ambao tunakaribia kukamilisha taratibu zote na muda sio mrefu tutaanza kuwatangaza rasmi kwa mashabiki zetu,” alisema Wendo.

Mkuu huyo wa mkoa, ni mlezi wa Mbuni ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu na Makalla alitangazwa kushika wadhifa huo rasmi tangu Oktoba 23, 2025, alipokutana na kuzungumza na menejimenti na wachezaji wa kikosi hicho.

Kwa sasa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid unatumiwa na timu za Mbuni na TMA zinazoshiriki Ligi ya Championship, huku mara ya mwisho kwa klabu ya Arusha kuuchezea kwa ajili ya Ligi Kuu ilikuwa ni JKT Oljoro iliyoshuka daraja msimu wa 2013-2014.