Mpole, Martin kuna jambo Tanzania Prisons

TANZANIA Prisons imefikia pazuri katika mazungumzo ya kuwasajili wachezaji watatu wa eneo la ushambuliaji ambao ni George Mpole, Emmanuel Martin na Gustavo Simon.

Chanzo cha ndani kutoka Prisons kilisema mazungumzo na wachezaji hao yalianza juzi na yamefikia pazuri, hivyo huenda wakasaini mkataba wa mwaka mmoja, wakiwatarajia wataongeza nguvu ya kuhakikisha timu inapanda nafasi za juu kutoka ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi saba kwa mechi saba.

Mpole aliyewahi kuibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17 msimu wa 2021-2022 kisha akaenda kujiunga na FC Lupopo ya DR Congo, hivi sasa ni mchezaji huru baada ya kuachana na Pamba Jiji aliyoitumikia msimu wa 2024-2025 na kufunga mabao mawili.

“Ukiachana na Mpole, kwa upande wa Martin aliyewahi kuichezea Yanga ana uzoefu tunaoamini utatufaa kwani tunahitaji ushindi ili tusirudie mapito ya msimu uliopita wa kucheza mechi za kujikwamua kushuka daraja,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kocha alihitaji wachezaji wengi akiwamo Tepsi Evance ambaye tunasikia kajiunga na JKT Tanzania, wengine Gadiel Michael na Ayubu Lyanga lakini siyo kila mazungumzo yanaweza yakafanikiwa.”

Chanzo hicho kilisema kwa wachezaji walioongezeka katika timu hadi sasa ni Samson Mbangula aliyekuwa amekaa nje akiuguza majeraha.