JUMLA ya makocha 16 wa mchezo wa gofu wamepata mafunzo kwa ajili ya kuwafundisha wachezaji chipukizi hapa nchini.
Mafunzo hayo Community Golf Instructor (CGI) yanaendeshwa na wakufunzi wa kimataifa kutoka Shirikisho la Gofu R&A kwa kushirikiana na Chama cha Gofu Tanzania (TGU na The Peninsula Club), yanalenga kuimarisha maendeleo ya mchezo huo hapa nchini hususan katika ngazi ya jamii na vijana.
Meneja wa Operesheni wa TGU, Johnson John, alisema mafunzo hayo yanafanyika kwenye klabu ya Peninsula, ambayo imeendelea kuwa mshirika muhimu wa TGU katika kutekeleza programu za kimkakati za kukuza gofu nchini.
John alisema kupitia ushirikiano huu, TGU na wadau wake wanajenga uwezo wa wakufunzi, makocha na waendelezaji wa gofu kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyotambuliwa na The R&A.
“Ushirikiano kati ya TGU, The Peninsula Club na The R&A unaakisi dhamira ya pamoja ya kukuza gofu kwa misingi endelevu, jumuishi, na yenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii. Mafunzo ya CGI ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha gofu inafundishwa kwa weledi, usalama, na kwa mtazamo wa maendeleo ya kizazi kijacho cha wachezaji,” alisema John.
Kwa upande wa mkufunzi, Pete Forster alisema amefurahishwa sana kuona Tanzania imepata mafanikio katika mchezo huo na kuamini kupitia mafunzo hayo, Tanzania itapanua wigo wa gofu hapa nchini.
“Tanzania ina vipaji vingi vya mchezo wa gofu ambavyo vinatakuwa kuendelezwa ili kufikia maendeleo ya juu kabisa hapa na kushindana kimataifa. Mafunzo haya yatazalisha wachezaji wengi chipukizi ambao watakuwa wamepata mafunzo kutoka kwa makocha hawa 16, nimefarijika sana,” alisema Forster.
Mbali ya Forster, wakufunzi wengine ni Alex Macgregor na Vincent Wang’ombe.
Mmoja wa makocha na mchezaji pekee wa gofu wa kulipwa kwa wanawake, Angel Eaton alisema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa zaidi ya ufundishaji ambayo watayatumia kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huo.
Eaton alisema mchezo wa gofu kama michezo mingine, inakuwa na kuwa na njia za kisasa za ufundishaji, jambo ambalo wanaishukuru TGU, R&A na The Peninsula Club kufanikisha mafunzo hayo.
Wachezaji wengine wa kulipwa, Salum Dilunga alisema kupitia mafunzo hayo, wataifikia jamii na kuibua vipaji Zaidi huku Geofrey Leverian akitoa wito kwa wazazi kuwaruhsu watoto wao kuanza kucheza mchezo huo.