KUMBUKUMBU tuliyonayo hapa kijiweni ni straika wa mpira, Paul Peter alishawahi kuonja hela za timu kubwa hapa nchini ingawa hazikuwa nyingi sana kwa vile alikuwa bado kinda wakati huo.
Ni kipindi alipopandishwa katika kikosi cha wakubwa cha Azam FC baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na timu yao ya vijana.
Hata hivyo, kutokana na uwingi wa wachezaji wengi wa nafasi ya ushambuliaji tena wazoefu na wakomavu kumzidi yeye kipindi hicho, Peter alishindwa kutoboa pale Azam na ikamlazimu akasake maisha kwingine.
Kama unavyojua pale Azam maisha ni ya raha na mazuri sana kwa wachezaji. Wanalipwa hela nyingi, wanalala pazuri na wanapata huduma zote stahiki ambazo mchezaji anatakiwa apatiwe tena kwa wakati hivyo kwa anayepita pale lazima awe na hamu ya kucheza hapo au timu kubwa nyingine.
Inaonekana Peter ambaye kwa sasa yupo JKT Tanzania, ameyakumbuka maisha ya timu kubwa na anataka kuutumia msimu huu kutengeneza mazingira ya kurejea ama Azam au Simba na Yanga.
Njia ya kurejea au kwenda katika timu hizo siyo nyingine bali ni kuonyesha kiwango katika mechi za timu yako ya daraja la kati au la chini kiuwekezaji ili uweze kushawishi vigogo vya soka vikunyakue kwa fungu kubwa la fedha katika dirisha la usajili.
Pale JKT Tanzania hivi sasa, Peter ndio amekuwa mshambuliaji kiongozi na anatoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa mabao ya Maafande hao kwenye Ligi .
Hadi sasa ameshausika na mabao nane ambapo amefumania nyavu mara tano na amepiga pasi tatu za mwisho jambo linalomfanya awe kinara wa kupachika mabao kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa.
Jamaa ameamua kucheza na namba tu maana anajua ndio njia rahisi ya kumfanya avune pesa nono katika dirisha lijalo la usajili.
Mabao yake yatafanya akaunti zake zijae noti muda sio mrefu.