CMA yaja na mkakati kuharakisha utatuzi migogoro kazini

Dar es Salaam. Suala la kusafiri kufuata mahakama kwa ajili ya utatuzi na usuluhishaji wa migogoro ya kazi halitakuwepo tena, baada ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa kidijitali wa e-Utatuzi, unaoruhusu usajili wa mashauri ya usuluhishi na uamuzi kwa njia ya mtandao.

Mfumo huo, uliozinduliwa jana Jumatano, Januari 21, 2026 jijini Dar es Salaam, unalenga kuondoa ucheleweshaji wa kesi na kupunguza gharama za kusafiri kwa wananchi wanaohitaji huduma za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema e-Utatuzi ni hatua ya kisasa inayolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kasi katika utoaji wa haki.

“Serikali inatambua umuhimu wa CMA kwa kuwa huduma zake zinagusa waajiri na waajiriwa, ambao wanachangia moja kwa moja ukuaji wa uchumi wa nchi. Bila CMA imara na yenye uwezo wa kutatua migogoro kwa haraka, uchumi unaweza kuathirika,” amesema.

Sangu amesema kwa sasa, mtu yeyote aliye na mgogoro wa kazi anaweza kuwasilisha malalamiko yake mtandaoni, kufuatilia maendeleo ya kesi na kupokea majibu bila kusafiri umbali mrefu.


Ameeleza mfumo huo unalenga kuhakikisha kuwa kesi zinashughulikiwa kwa haraka na kwa uwazi, hatua inayotarajiwa kuboresha uhusiano wa kazi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Dk Yose Mlyambina, amesema mfumo huo utaongeza ufanisi na uwazi katika utatuzi wa migogoro.

Amesema teknolojia hiyo itarahisisha utaratibu wa mashauri na kuhakikisha kila kesi inashughulikiwa kwa wakati.

Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla, amesema e-Utatuzi ni kielelezo cha maendeleo ya kidijitali.


Amesema mfumo huo utarahisisha utoaji huduma, kuongeza uwazi na kutoa takwimu muhimu zitakazosaidia kuboresha sera za utatuzi wa migogoro ya kazi nchini.