Familia yagoma kuzika mwanafunzi anayedaiwa kukatwa na jembe shuleni

Shinyanga. Mwanafunzi Kassim Omary (12) wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Bukindwasali iliyopo Ushetu mkoani Shinyanga, amefariki dunia akidaiwa kukatwa kichwani na jembe wakati anachimba mchanga.

Tukio hilo lilitokea Januari 21, 2026 wakati wanafunzi hao wakichimba mchanga kwa ajili ya ukarabati wa darasa uliokuwa ukiendelea shuleni hapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amethibitisha tukio hilo na mwanafunzi kuwa huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Zahanati ya Nyankende.

Kamanda Magomi amesema wakati wanafunzi hao wakiendelea na shughuli hiyo, Kassim alikuwa shimoni na mwenzake (jina tunalo) alikuwa akichimba eneo la juu, ndipo jembe la mwenzake lilipoteleza na kumkata Kassim kichwani.
Amesema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo.

“Mwanafunzi huyu pamoja na wenzake walitumwa kufuata mchanga kwa ajili ya ujenzi uliokuwa ukiendelea shuleni, huyu Kassim alitumbukia shimoni, juu alikuwepo mwenzake ambaye aliteleza na jembe lake likaangukia kule shimoni na kumkata mwenzake kichwani.”

Kamanda Magomi ametoa wito kwa walimu kuwafuatilia wanafunzi wanapokuwa katika kazi za mikono shuleni ili kuzuia majanga kama hayo.
 

Baba mzazi wa marehemu, Omary Masolwa amesema siku ya tukio mwanawe alienda shule na baada ya muda alirudi nyumbani na kumweleza kuwa wameagizwa vifaa vya kubebea mchanga, akampatia kisha akarudi shule.

Amesema mtoto wake alikuwa na kawaida ya kurudi nyumbani saa nne asubuhi kunywa uji, lakini siku hiyo hakurudi hadi alipopata taarifa kuwa amekatwa na jembe kichwani.

“Saa saba nikaona mtoto wa jirani anakuja anakimbia, akaniambia Kassim mwanao amekatwa na jembe. Na nani? Na mwanafunzi mwenzie. Wapi? Kichwani. Anatembea? Hapana damu zinatoka nyingi ameanguka chini.”

Amesema alienda shuleni na baada ya kufika, aliambiwa asubiri kwani kuna mwalimu alienda eneo la tukio lakini baada ya muda mwalimu huyo alipiga simu akiomba msaada kwa walimu wenzake, ndipo wakaenda huko.

“Kabla sijafika nikamuona mwanangu amebebwa na wanafunzi wenzie, kufika hapa shuleni wakaanza kumpepea tu lakini bado mtoto yuko mahututi, nikamwangalia tu mara moja nikajua hapa mtoto hayupo, nimelia sana, nimeshindwa hata kumwangalia mtoto.”

Amesema baada ya muda mtoto alipelekwa zahanati ya Nyankende, na baadaye wakifanya taratibu za kumpeleka Kituo cha Afya Bulungwa ndipo alipopewa taarifa za msiba.

“Zahanati ya Nyankende wakasema tumkatie rufaa aende Bulungwa, gari ikafika, sasa ikawa mizunguko tu hapa, mara waniambie twende Kahama, mara Bulungwa, au Nyamilangano, kumbe mtoto wangu ameshakufa wanatafuta namna ya kuniambia,” amesema Masolwa

“Hatutazika mpaka tujue imekuwaje mpaka mwanangu awe maiti, hawa watoto kwenye kuchimba mchanga walikuwa wenyewe hamna hata mwalimu, polisi ndo wamefika sasa hivi hapa nyumbani.”

Mwananchi ilitamfuta tena Kamanda Magomi kuhusu uamuzi wa familia hiyo kukataa kuzika, akasema kuhusu suala hilo atatoa taarifa baadaye.