Na Oscar Assenga,TANGA
BENKI Kuu ya Tanzania (BOT) imesema kwamba taasisi ndogo zinazotoa huduma za kubadilisha fedha za kigeni nchini zinapaswa kusajiliwa ili ziweze kupata leseni ya kuendesha shughuli zao,kinyume na hapo ni kosa kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Afisa Mwandamizi Mkuu kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mwile Kauzeni wakati alipokuwa akizungumzia na Waandishi wa habari kwenye viwanja vya Usagara Jijini Tanga, eneo ambalo Maadhimisho ya Wiki ya fedha kitaifa yanafanyika mwaka huu.
Mwile alikuwa akijibu Swali la Wanahabari waliotaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na benki kuu ya Tanzania katika kudhibiti Watu wanaoendesha biashara ya kubadilisha fedha kiholela.
Ambapo badala yake aliwasihi kufuata Sheria hatua ambayo itawawezesha kupata inayoruhusu uendeshaji kazi hiyo.
Alisema kuwa, ili mtu kufanya biashara hiyo anapaswa kufuata taratibu za kisheria kwa vile kinyume chake atakuwa ametenda kosa la jinai ambapo amewataka wale wenye nia kuendesha shughuli hiyo kutembelea matawi yake.
Aidha alisema taasisi ndogo za huduma za fedha zinahitaji kusajiliwa ili kuweza kupata leseni BOT kutokana na kwamba kubadilisha fedha bila leseni ni kosa kisheria
Awali akizungumza Afisa Mchambuzi Masuala ya Fedha wa BOT Charles Kanuda alisema kwamba, Serikali imekuja na mfuko wa udhamini wa mikopo ambapo kwa mtanzania anayehitaji mkopo huku akiwa hana dhamana toshelevu atapata dhamana mpaka asilimia 75.
Kanuda alisema kwamba,watu wengi wamekuwa wakijaribu kwenda kukopa huku wakiombwa dhamana yenye thamani kubwa zaidi ya mikopo wanayohitaji na hivyo kushindwa kupata mikopo.
Amesema kwamba hali hiyo imewasababisha watanzania walio wengi kushindwa kuchukua mikopo au kuchukua kiasi kidogo jambo ambalo limeathiri ufanisi wa biashara zao wanazoziendesha.
Katika maadhimisho haya ya wiki ya fedha kitafa yenye kauli mbiu ya ” elimu ya fedha , msingi wa Maendeleo ya kijamii na kiuchumi” Wadau mbalimbali walitembelea na kupatiwa elimu banda la BOT.
Mwajuma Kileo ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkwakwani Jijini Tanga, yeye alielezea kuridhishwa kwake na elimu aliyoipata baada ya kutembelea banda hilo la BOT.
Alisema kwamba, kwa kutembelea banda hilo alijifunza namna ya kutambua fedha bandia mambo ambayo pia walikuwa wakiwafundisha wanafunzi kupitia somo la uraia wanapokuwa Shule.
Adrus Mahmoud (12) mwanafunzi wa darasa la sita kwenye Shule hiyo ya Mkwakwani,alisema amefarijika kupatiwa elimu ya ziada juu ya kutambua alama za kificho zilizomo kwenye noti na hivyo kumsaidia kubaini zilizo za bandia.