Trump aanzisha ‘Bodi ya Amani’ kuchukua nafasi ya UN, dunia yagawanyika

Dar es Salaam. Kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba chombo kipya alichokianzisha cha “Bodi ya Amani” kinaweza kuchukua nafasi ya Umoja wa Mataifa (UN), imezua taharuki katika medani ya diplomasia ya kimataifa na kuibua mjadala juu ya mwelekeo mpya wa usimamizi wa masuala ya amani na usalama duniani.

Hatua hiyo imewakosesha usingizi washirika wa karibu wa Marekani, ambao wameanza kuonesha wasiwasi mkubwa kuhusu dhamira halisi ya bodi hiyo, uhalali wake kisheria na athari zake kwa taasisi za kimataifa zilizoanzishwa kwa miongo kadhaa.

Hofu kubwa imeelekezwa katika mustakabali wa UN iliyoanzishwa mwaka 1945 mjini San Francisco, Marekani, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kwa lengo la kuimarisha amani, usalama na ushirikiano wa kimataifa.

Kuanzishwa kwake kulilenga kuchukua nafasi ya League of Nations, iliyoshindwa kuzuia kuzuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kutokana na udhaifu wa kimuundo, ukosefu wa mamlaka ya kisheria na kushindwa kuyashirikisha mataifa yenye nguvu duniani.

Kupitia Mkataba wa Umoja wa Mataifa uliosainiwa na nchi 51, UN ilipewa mamlaka mapana zaidi ya kisiasa na kisheria, yakiwemo Baraza la Usalama lenye wajumbe wa kudumu, ili kuhakikisha migogoro ya kimataifa inatatuliwa kwa njia za amani na kuzuia dunia kurudia maafa ya vita vikubwa.

Pia, kwa mara ya kwanza, Marekani kama taifa lenye nguvu duniani ilijiunga uanachama wa Umoja wa Mataifa.

Bodi hiyo, ambayo awali ilipangwa kusimamia ujenzi wa Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita, sasa inaonekana kupanua wigo wake hadi kushughulikia migogoro ya dunia nzima.

Hatua hiyo, pamoja na ukweli kwamba Trump atakuwa mwenyekiti wake wa kudumu bila ukomo wa muda, imeibua hofu kuwa bodi hiyo inalenga kuipiku UN.

Kwa mujibu wa rasimu ya katiba ya bodi hiyo, Trump ataendelea kuwa mwenyekiti hata baada ya kumaliza muhula wake wa pili wa urais, na ataondolewa tu kwa kujiuzulu mwenyewe au endapo wajumbe wote wa bodi watakubaliana kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake.

Ikulu ya White House imetangaza “Bodi ya Utendaji ya Waanzilishi” itakayomsaidia Trump, ikijumuisha mkwe wake Jared Kushner, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, mjumbe maalumu Steve Witkoff, pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.

Trump ametuma mialiko kwa takribani mataifa 50 kujiunga na Bodi ya Amani, huku karibu nchi 35 zikitarajiwa kuhudhuria hafla ya kusaini makubaliano hayo leo, Alhamisi, Januari 22, 2026, pembezoni mwa mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos.

Baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati, kama Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Misri, Qatar na Bahrain, tayari yamekubali kujiunga.

Hata hivyo, mataifa kadhaa ya Ulaya yamekataa au kuonesha kusita.

Ufaransa na Norway zimesema hazitashiriki kwa sasa, zikieleza wasiwasi kuhusu jinsi bodi hiyo itakavyofanya kazi sambamba na UN.

Italia imetaja changamoto za kikatiba, huku Ireland ikisema itachunguza kwa kina kabla ya kutoa msimamo wake.

Russia, China na utata wa uanachama

Miongoni mwa mataifa yaliyoalikwa kujiunga ni Russia, China na Belarus, hatua iliyozua ukosoaji mkali, hasa kutokana na vita vinavyoendelea Ukraine.

Trump amedai kuwa Rais wa Russia, Vladimir Putin, amekubali mwaliko huo, ingawa Moscow imesema bado inachambua nyaraka husika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, alisema wazi kuwa Putin “si mtu wa amani,” akionya kuwa ushiriki wa Russia unaweza kudhoofisha UN na kuongeza migawanyiko miongoni mwa washirika wa Magharibi.

Israel pia imekubali kujiunga kupitia Waziri Mkuu wake, Benjamin Netanyahu, licha ya kukosolewa kimataifa na kuwepo kwa hati ya kukamatwa dhidi yake kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Ufaransa na Norway zimetangaza kutoshiriki kwa sasa, zikieleza kuwa mpango huo una maswali mengi kuhusu uhalali wake kisheria na uhusiano wake na UN.

Italia pia imesema haitahudhuria hafla ya utiaji saini, ikitaja mgongano wa kikatiba.

Ada ya Dola bilioni 1, lawama za ‘klabu binafsi’

Kwa mujibu wa utaratibu uliopendekezwa, nchi wanachama watatumikia kwa kipindi cha miaka mitatu, lakini zitahitajika kulipa Dola bilioni moja ili kupata kiti cha kudumu.

Serikali ya Marekani imesema fedha hizo zitaelekezwa kwenye ujenzi mpya wa Gaza, ingawa wakosoaji wanasema mfumo huo unafungua mianya ya rushwa na upendeleo.

Wachambuzi wa diplomasia wamefananisha mpango huo na “klabu binafsi ya matajiri,” wakisema si kila taifa lenye uwezo wa kifedha linafaa kuamua masuala nyeti ya amani na usalama wa dunia.

Maofisa wa UN wamepunguza uzito wa kauli za Trump, wakisisitiza kuwa taasisi hiyo haitakufa.

Pia, msemaji wa Naibu Katibu Mkuu wa UN alisema kuwa kuna taasisi nyingi zimekuwepo sambamba na UN kwa miongo kadhaa, lakini mamlaka ya kulinda amani ya dunia bado ni ya kipekee kwa UN.

Kwa sasa, hatima ya Bodi ya Amani inaonekana kutegemea zaidi iwapo itaweza kuleta mafanikio ya kweli katika ujenzi wa Gaza.

Bila hilo, wachambuzi wanaonya kuwa bodi hiyo inaweza kubaki kuwa mradi tata wa kisiasa unaoongeza migawanyiko badala ya kuleta amani ya kudumu duniani.