Wawili wafutiwa kesi na DPP, tisa waendelea kusota tuhuma wizi wa Sh5.7 bilioni

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia kesi ya uhujumu uchumi na kuwaachia huru washtakiwa wawili kati 11 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka  ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.

Mahakama hiyo imewafutiwa mashtaka yao, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kesi dhidi ya washtakiwa hao wawili.

Waliofutiwa mashtaka na kuachiwa huru ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Caroline Masayanyika ambaye alikuwa ofisa wa benki hiyo kutoka makao makuu ya benki hiyo na mshtakiwa wa 10 katika kesi hiyo Claude Beda, ambaye ni mfanyabiashara.

Washtakiwa ambao wanaendelea na kesi hiyo ni Jasmine Elphas ambaye alikuwa ni ofisa wa Benki ya Equity makao makuu na mfanyabiashara Fredrick Elphas Ogenga.


Wengine ni Lilian Koka, ambaye alikuwa ofisa wa benki hiyo kutoka makao makuu ya benki hiyo.

Vile vile, yupo  Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.

Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7bilioni kwa udanganyifu mali ya Benki ya Equity Tanzania Limited.

Leo, Wakili wa Serikali Mkuu, Caren Mrango akishirikiana na wakili wa Serikali Titus Aron, ametoa taarifa hiyo mbele ye Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

” Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya kutajwa, lakini tunaomba kuitaarifu mahakama kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini hana nia ya kuendelea kumshtaki mshtakiwa wa tatu na mshtakiwa wa 10 katika kesi hii, hivyo tunaiomba mahakama yako iwaondolee mashtaka,” alisema wakili Mrango.

Mrango ameieleza Mahakama hiyo kuwa  DPP amewasilisha hati ya kutokuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa  hao wawili, chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023.

“Pia, tunaomba  kuitaarifu Mahakama hii kuwa tupo katika hatua za mwisho za upelelezi wa jalada hili na muda wowote kuanzia sasa tutaweza kusajili taarifa muhimu  katika Mahakama inayofaa( Mahakama Kuu), hivyo kutokana na sababu hizi, tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” alidai Mrango.

Jamhuri baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili Steven Mosha na Meshack Dede wanaowatetea washtakiwa watano ambao ni Jasmine, Ogenga, Fata, Paul na Jefferson waliitaarufu mahakama kuwa wateja wao wameingia majadiliano ya kuimaliza kesi.

Kwa upande wake mshtakiwa wanne katika kesi hiyo, Lillian Koka yeye anatetewa na wakili Godian Mgusi.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na ombi la upande wa mashaka na kuahirisha kesi hadi Februari 4, 2026 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Kwa pamoja wanakabiliwa na Uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya jijini Dar es Salaam,  waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.

Katika tarehe hizo mshtakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya Makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika akaunti ya clearing and settlement mali ya benki ya Equity.

Mshtakiwa Caroline katika tarehe hizo, akiwa katika Makao Makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, anadaiwa kuiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.


Pia, ilidaiwa, kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 makao makuu ya benki hiyo, Lilian  aliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.

Vile vile, kati ya Januari Mosi hadi Aprili 24, 2025 katika benki hiyo, Maina aliiba Sh101 milioni  mali ya benki hiyo.

Ilidaiwa, kati ya Januari 22 hadi Aprili 24, 2025 katika ofisi hizo za benki hiyo  Mohamed aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2 ,2024 hadi Mei 25, 2025

Mahakama ilieleza kuwa, kati ya Januari 9, hadi Mei 25, 2025,  Makao Makuu ya Benki ya Equity iliyopo Ilala, Mrisho aliiba Sh211 milioni, mali ya benki hiyo.

Upande wa mashtaka ulidai, kati ya Januari 9 hadi Mei 28,2025  makao makuu ya benki hiyo, mshtakiwa Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki hiyo.

Vile vile siku na eneo hilo, Beda anadaiwa kuiba Sh108 milioni, mali ya benki hiyo.

Pia, ilidaiwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 10 ya utakatishaji wa fedha walizodaiwa kuiba.