Kumbukizi maisha ya Mtei yaahirishwa, sababu zatajwa

Arusha. Kumbukizi ya maisha ya Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), marehemu Edwin Mtei iliyokuwa imepangwa kufanyika kesho Ijumaa Januari 23, 2026, imeahirishwa ili kupisha maandalizi ya ibada ya maziko.

Mtei (94), atazikwa nyumbani kwake eneo la Tengeru, mkoani Arusha, Jumamosi Januari 24, 2026.

Mtei alizaliwa Julai 12, 1932, Marangu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro na alifariki dunia usiku wa Januari 19, 2026, akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Selian kwa matibabu.

Akizungumza leo Alhamisi, Januari 22, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, amesema kumbukizi hiyo iliyokuwa ifanyike kesho imeshindikana baada ya familia kueleza kuwa siku hiyo itatumika kuandaa ibada ya maziko katika eneo lilelile lililopangwa kufanyika kumbukizi hiyo.

Amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao vya pamoja kati ya chama na familia ya marehemu.
“Baada ya familia kufanya kikao, walitueleza kupitia msemaji wao kuwa kumbukizi haitawezekana kufanyika Ijumaa kwa sababu eneo hilo litakuwa linaandaliwa kwa ajili ya ibada ya maziko,” amesema Golugwa.

Amesema kutokana na Jumamosi kuwa ndiyo siku ya maziko, ni vigumu kuandaa kumbukizi katika muda huo.

Hata hivyo, Golugwa amesema Chadema kinaendelea kushauriana na viongozi wake kuona namna bora ya kulitekeleza suala hilo baadaye.

Amesema viongozi wakuu watano wa Chadema, isipokuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Tundu Lissu aliyeko mahabusu, pamoja na wajumbe 11 wa Kamati Kuu, wamethibitisha kushiriki maziko ya mwasisi huyo.

Aidha, amesema viongozi wa kanda zote 10 za chama pamoja na viongozi wa mikoa wanatarajiwa kushiriki kumpumzisha mwasisi huyo wa Chadema.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari jana msibani, Golugwa alisema ujumbe maalum kutoka kwa Lissu akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga ulikuwa umepangwa kusomwa wakati wa kumbukizi hizo.

Amesema chama kilimtuma Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Garubindi kwenda kuuchukua ujumbe huo gerezani kwa ajili ya kuja kusomwa kama sehemu ya kumuenzi marehemu Mtei, ambaye pia alikuwa mkulima mkubwa wa kahawa.

Kwa upande wake, msemaji wa familia ya marehemu na mwenyekiti wa zamani wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema  maandalizi ya maziko yanaendelea nyumbani kwa marehemu Tengeru na maeneo ya jirani.

Akizungumzia mwenendo wa msiba huo, Mbowe amesema ni wa kitaifa na shirikishi kutokana na mchango mkubwa wa marehemu katika historia ya nchi kabla na baada ya uhuru, ndani ya Serikali, taasisi za kitaifa na kimataifa.

“Huu ni msiba wa Watanzania wote. Marehemu amehudumu katika nyanja mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Familia iko tayari kushirikiana na kila mtu kuhakikisha anapata nafasi ya kumuenzi baba huyu,” amesema Mbowe.

Kuhusu kumbukizi ya maisha ya marehemu iliyopangwa kufanywa na Chadema, Mbowe amesema familia na chama bado wanaendelea kutafuta njia bora ya kuhakikisha simulizi na mchango wa Mtei katika historia ya Chadema na taifa unaenziwa ipasavyo.

Edwin Mtei aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo kuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania kuanzia mwaka 1966.

Miaka 12 baadaye, aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango kuanzia mwaka 1978 hadi 1981, alipojiuzulu wadhifa huo.

Kwa sasa, msiba unaendelea nyumbani kwake Tengeru, Arusha, huku mipango ya mazishi ikiendelea.