NAIBU WAZIRI LONDO AITAKA WMA KUSIMAMIA SHERIA KULINDA HAKI ZA MLAJI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, ameitaka Wakala wa Vipimo (WMA) nchini kuongeza uwajibikaji katika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria ya Vipimo ili kuwalinda walaji dhidi ya udanganyifu na kuhakikisha wanapata bidhaa na huduma kulingana na thamani halisi ya fedha zao.

Londo amesema usimamizi madhubuti wa vipimo ni msingi muhimu katika kujenga uchumi shindani, himilivu na jumuishi, sambamba na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala wa Vipimo katika Kituo cha Uhakiki wa Vipimo Misugusugu Mkoa wa Pwani, ambapo amesisitiza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga kuhakikisha kunakuwepo na mazingira wezeshi ya biashara huku ikijenga imani kwa walaji katika huduma na bidhaa wanazopata.

Naibu Waziri ameongeza kuwa kutokuwepo kwa usimamizi sahihi wa vipimo kunawanyima walaji haki zao za msingi na kudhoofisha ushindani wa haki katika biashara, jambo linaloweza kuathiri ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Bw. Alban Kihulla amewasihi Wananchi kushirikiana na Wakala huo kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini kupatiwa huduma kwa kutumia vipimo visivyo sahihi, akisema ushirikiano wa Wananchi ni nyenzo muhimu katika kudhibiti vitendo vya udanganyifu na kuimarisha haki katika biashara.

Wakala wa Vipimo ina jukumu la kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakuwa sahihi kwa mujibu wa Sheria, hatua inayolenga kulinda maslahi ya walaji na kukuza biashara nchini.