Wataalamu wamekuja na majibu yatakayomaliza mgogoro wa mipaka baina ya kijiji cha Rudewa Mbuyuni kilichopo kata ya Rudewa na kijiji cha Mbwade kilichopo kata ya Madoto wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Ahueni ya mgogoro huo imepatiwa ufumbuzi baada ya kufanya tathimini na kuja na ripoti inayoonesha uhalisia wa mipaka ya vijiji hivyo.
Tathmini hiyo imeonesha uhalisia kuwa eneo kubwa la Kijiji cha Rudewa Mbuyuni ambalo lilikuwa likidhaniwa ni lao lipo ndani ya Kijiji cha Mbwade.
Akisoma taarifa hiyo kwenye mkutano wa hadhara baina ya Mkuu wa Wilaya hiyo Shaka Hamdu Shaka na wakazi wa Kijiji cha Rudewa Mbuyuni, Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Hamisi Hilal amesema kuwa kwa mujibu wa ramani yenye usajili namba 66277 iliyoidhinishwa na Wizara ya Ardhi mwaka 2011, iliyotumika kwenye tathimini hiyo inaonesha Kijiji cha Rudewa Mbuyuni kina ukubwa wa hekta 3,228.003 na Kijiji cha Mbwade kina ukubwa wa hekta 1,392.77, huku eneo lenye mgogoro likiwa ni hekta 1,483.
“Shughuli ya upimaji na uhakiki wa mipaka ya vijiji vyote limefanyika hadi kufika kwenye eneo lenye alama ya mpaka wa mwisho na ilionesha uhalisia kuwa eneo kubwa la Kijiji cha Rudewa Mbuyuni lililokuwa likigombaniwa lipo katika Kijiji cha Mbwade,” amesema Hilal.
Akizungumza baada ya kuwasilishwa ripoti hiyo, Shaka amesema kwa kuwa ripoti hiyo ni rasmi hayo ndiyo maamuzi ya Serikali juu ya mgogoro huo ambapo yatasimamiwa na kuheshimiwa na kila mmoja.
Amesema ripoti hiyo pia itawasilishwa kwa wakazi wa Kijiji cha Mbwade ili nao wafahamu maamuzi yaliyofikiwa na Serikali baada ya timu ya wataalamu kufanya uhakiki wa kina, kabla ya hatua nyingine inayofuata ya kufikia maamuzi ya mwisho ya utatuzi wa mgogoro huo.
Ameisisitiza kuwa Serikali haina mpango wa kuwaondoa watu waliopo kwenye eneo hilo, bali mipango iliyopo ni kufanya uhakiki wa watu waliopo kwenye maeneo hayo ili kupata suluhu ya kudumu itakayosaidia kuondoa uhasama uliopo baina yao, na kuwezesha shughuli za kijamii kuendelea katika eneo hilo lenye mgogoro.
“Mbwade ni watu wetu na Rudewa ni watu wetu. Sisi kazi yetu ni kusimamia haki, usawa na ukweli ili kusudi amani iweze kutawala. Mlihitaji tufanye kazi hii, tumeifanya kwa uaminifu na ustadi kwa kushirikisha timu za wataalamu kwenda mbali zaidi na niwaambie kuwa haya ndiyo maamuzi ya Serikali kwenye mgogoro huu,” amesema Shaka.
Shaka ameongeza kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayetumia mgogoro huo kuhatarisha usalama na kueneza uchochezi miongoni mwa wakazi wa vijiji hivyo viwili, wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kutafuta suluhu ya kudumu.
Aidha, amesema kuwa kwa kiasi kikubwa kiini cha mgogoro huo ni uzembe wa viongozi wa Kijiji cha Mbuyuni, ambao wamekuwa wakihusishwa kutumia maeneo hayo kujinufaisha wenyewe, ikiwemo kuuza kwa watu wengine pasipo kufuata sheria, pamoja na kutowaeleza wananchi wao taarifa sahihi juu ya uhalisia wa eneo la kijiji chao.
Kwa upande wake, mmoja wa wakazi wa eneo hilo lenye mgogoro, Asteria Charles, amesema kuwa tangu mwaka 2010 alipofika alikabidhiwa sehemu ya kulima na Kamati ya Kijiji cha Mbuyuni, ambalo amekuwa akilitumia kufanya shughuli za kilimo hadi sasa.