WIZARA YAKUTANA NA KAMATI YA MAMBO YA NJE BUNGE

:::::

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameongoza Menejimenti ya Wizara katika kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kilichofanyika katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.

Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb.) kililenga kujadili masuala mbalimbali ya utendaji wa Wizara na kuangazia hali ya ushirikiano wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikanda na kimataifa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na hali ya ushirikiano wa Tanzania katika Jumuiya za kikanda Mhe. Waziri Kombo alieleza juu ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge yanayohusu sekta ya mambo ya nje, ikiwemo utekelezaji wa diplomasia ya uchumi inayolenga kulinda maslahi ya Taifa katika nyanja za kiuchumi.


Katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mhe. Najma Murtaza Giga amempongeza Waziri Kombo na Menejimenti ya Wizara kwa kazi nzuri inayofayika na kuitaka Wizara kuchukua hatua za kimkakati katika kutumia fursa zilizopo ili kukuza ushirikiano wa kimataifa, hususan katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Amesema ni muhimu kwa Wizara kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa ufanisi ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na fursa zilizopo nje ya nchi, ikiwemo kuvutia uwekezaji, nafasi za ajira, kukuza biashara na kulinda maslahi ya Taifa katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Kamati imeishauri Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuweka mkazo zaidi kwenye Diplomasia ya Uchumi, ili kuhakikisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inanufaika ipasavyo na fursa zinazopatikana kupitia diplomasia ya uchumi.

Wajumbe wa Kamati hiyo, wameeleza umuhimu wa kutekeleza diplomasia ya Uchumi kwa kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini, nafasi za ajira nje na ufadhili wa mafunzo nje ya nchi na kulinda maslahi ya Taifa katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.