Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba amesema hakuna kikwazo kwa mwananchi aliyejiajiri kujiunga na mfuko huo.
Amesema maboresho makubwa yaliyofanywa yamewawezesha wanachama wa kundi hilo kunufaika na mafao mbalimbali, sawa na waajiriwa wa sekta ya umma na binafsi.
Mshomba ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 22, 2026 alipowaongoza wafanyakazi wa NSSF kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama wapya katika soko la Tegeta Nyuki, jijini Dar es Salaam, kupitia kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi.
Amesema mwananchi aliyejiajiri atakayechagua kujiunga na NSSF, atanufaika na mafao ya pensheni ya uzeeni, urithi, ulemavu, uzazi, matibabu pamoja na mafao mengine ambayo hapo awali, hayakuwalenga moja kwa moja wanachama wa kundi hilo.
“Tunaposema wanachama wa NSSF ni mastaa wa mchezo, tunamaanisha kuwa Mfuko unatoa uhakika wa maisha bora, huduma za matibabu na kipato hata pale mwanachama anapostaafu. Endapo mwanachama atafariki, wategemezi wake watanufaika na mafao ya urithi,” amesema Mshomba.
Ameongeza kuwa NSSF imeboresha mfumo wa uchangiaji kwa kuufanya kuwa rahisi na rafiki kwa wananchi.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema mwanachama anayechangia Sh30,000 kwa mwezi, atanufaika na mafao yote ikiwamo matibabu, huku anayechangia Sh52,200 kwa mwezi atanufaika sambamba na mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne.
Mshomba amefafanua kuwa uchangiaji huo si lazima ufanyike kwa mkupuo mmoja, bali unaweza kufanywa kwa utaratibu wa kila siku, kila wiki, kila mwezi au kwa misimu, kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali, bila ulazima wa kufika katika ofisi za NSSF.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Omary Mziya amewahimiza wananchi waliojiajiri kujiunga na mfuko huo na kuchangia kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Naye Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele amesema kampeni ya NSSF Staa wa Mchezo Paka Rangi itaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko hilo, Katibu wa Soko la Tegeta Nyuki, Omary Hemed ameishukuru NSSF kwa kuendelea kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii sokoni hapo na kuwapa fursa wajasiriamali kujiunga na kuchangia.
Amesema wengi tayari wananufaika na mafao yanayotolewa, yakiwamo ya matibabu.