Dar es Salaam. Wataalamu wa lishe na viongozi wa Serikali wamependekeza kuanzishwa kwa sheria zitakazolazimisha wazazi kuchangia chakula cha watoto wao shuleni.
Mapendekezo hayo yametolewa leo Alhamisi Januari 22, 2026, jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa Tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa mwaka 2024/25.
Wametoa mapendekezo hayo kufuatia wito wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe kuzitaka mamlaka za mikoa, halmashauri na wadau wa maendeleo kutoa maoni kuhusu nini kifanyike ili Serikali na wadau washirikiane kikamilifu kutokomeza matatizo ya lishe nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Nyakia Chirukile amesema takribani asilimia 80 ya afua za lishe zinawahusu moja kwa moja wazazi, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu kwa kuwa unategemea hiari.
Amependekeza kuandaliwe sheria ndogo zitakazowawajibisha wazazi kuchangia chakula cha watoto wao shuleni.
“Kama ambavyo kuna sheria ya elimu inayomtaka mzazi kuwajibika kwa mtoto wake, suala la chakula nalo ni muhimu na linapaswa kuwapo wajibu wa moja kwa moja kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Amesema hali ya sasa inasababisha baadhi ya watoto kupata chakula shuleni huku wengine wakikosa kutokana na wazazi wao kushindwa kuchangia.
“Tumeona watoto wengine wanapelekewa chakula na wazazi wao shuleni na wanakula, lakini wengine hawali kwa sababu wazazi hawapeleki chakula,” amesema.
Mtaalamu wa Lishe kutoka Taasisi ya Nutrition International, Laureta Lucas amesema licha ya maboresho makubwa yaliyofanyika katika kushughulikia lishe ya watoto chini ya miaka mitano na wajawazito, kundi la vijana balehe bado halijapewa kipaumbele cha kutosha.
Amesema tafiti zinaonesha shule hazitumiki ipasavyo kama nyenzo ya kuboresha lishe ya vijana hao.
“Pamoja na jitihada za kutoa chakula shuleni, ni muhimu kuangalia pia masuala ya usalama wa chakula. Kutoa chakula pekee hakutoshi, chakula kinapaswa kuwajenga watoto kiafya na kiakili,” amesema.
Lucas amesema matumizi bora ya shule katika afua za lishe, yanaweza kusaidia kupunguza matatizo ya upungufu wa damu na udumavu miongoni mwa watoto na vijana.
Akichangia hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Tumaini Mikido amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa mipango jumuishi ya lishe si sera au mikakati, bali ni ukosefu wa fedha za kutosha.
Mikido amesema fedha zinazotengwa kwa ajili ya lishe katika halmashauri hazikidhi mahitaji halisi ya utekelezaji wa mipango hiyo.
“Tumejitahidi kufanya vizuri katika halmashauri, lakini shilingi 1,800 kwa mwananchi haitoshi kuakisi utekelezaji wa mpango mzima wa lishe wa halmashauri. Kuna haja ya Serikali Kuu kuongeza fedha kupitia bajeti yake,” amesema.
Mtaalamu wa Lishe, Omary Gwao amesema ushirikiano wa kitaalamu kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini ni muhimu ili kuleta matokeo chanya.
“Katika uratibu wa afua za lishe, ni muhimu kuangalia namna ya kujumuisha makundi mbalimbali ya vyakula ili kupata matokeo makubwa zaidi,” amesema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya lishe kutokana na mitazamo potofu iliyopo katika baadhi ya jamii.
“Katika baadhi ya jamii, mtu mwenye kitambi anaonekana ana afya bora, wakati huenda ana utapiamlo au anaelekea kwenye udumavu. Ili kubadili mtazamo huu, elimu ya lishe inahitajika kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Myenzi amesema wataalamu wa lishe wana jukumu kubwa la kuelimisha jamii kuhusu ulaji bora unaozingatia uwiano sahihi wa vyakula.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema ajenda ya lishe inapaswa kupewa uzito wa kudumu katika vikao vya vijiji, mitaa na wazazi.
“Ni muhimu ajenda ya lishe iwe ya kudumu ili kuhakikisha kunakuwa na mafanikio. Hata katika vikao vya wazazi, suala hili linapaswa kujadiliwa ili kuwe na mipango ya pamoja,” amesema Mtatiro.
Amesisitiza kuwa, wazazi hawapaswi kuishia kuwaona watoto wanakwenda shule pekee, bali wahakikishe pia watoto wanapata chakula cha kutosha shuleni.
“Serikali imewekeza kwenye miundombinu ya elimu, lakini wazazi wasisahau kuwa mtoto anahitaji kula shuleni wakati wote anapokuwa nje ya nyumbani,” amesema mkuu huyo wa wilaya.