Watumiaji Stendi ya Magufuli walia ukosefu wa maji

Dar es Salaam. Watumiaji wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam wanakabiliwa na hofu ya magonjwa ya mlipuko kutokana ukosefu wa majisafi ulioanza tangu Desemba mwaka jana.

Imeelezwa  kuwa, kukosekana huduma hiyo mara kwa mara kunasababisha vyoo kukosa maji hali inayolazimu baadhi ya abiria, wafanyabiashara na watumiaji wengine kujisaidia ovyo, hivyo kuhatarisha afya na usalama wa mazingira ya stendi hiyo.

Hata hivyo, leo Alhamisi Januari 22, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire amesema uongozi wa mamlaka hiyo unaendelea kufuatilia changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo kupitia kwa mameneja ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Bwire amesema kutokana na ukubwa wa Jiji la Dar es Salaam, si rahisi kufuatilia changamoto za kila eneo moja kwa moja, hivyo jukumu hilo hufanywa na mameneja waliopo kwenye maeneo husika.

“Kupata taarifa za changamoto katika eneo moja moja kunanilazimu kurejea kwa meneja anayehusika, kwani Dar es Salaam ni kubwa na kila meneja anawajibika kusimamia eneo lake,” amesema Bwire.

Amesema uzalishaji wa maji unaendelea kama kawaida, na iwapo kuna maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo, mameneja wanaendelea kubaini, ikiwamo eneo la Stendi ya Magufuli.

Bwire amesema maeneo ya vituo vya mabasi (standi) si maeneo ya kawaida, hivyo ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa wakati wote kutokana na mkusanyiko wa watu.

“Standi si eneo la kawaida, ni lazima maji yapatikane muda wote kwa kuwa kuna mkusanyiko mkubwa wa watu,” amesema.

Jana, Jumatano, Januari 21, 2026 Mwananchi imezungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Aron Kagurumjuli amesema halmashauri imeanza kuchimba kisima kipya baada ya kile kilichopo kushindwa kuzalisha maji ya kutosha kukidhi mahitaji.

“Hadi sasa ninapozungumza na wewe, tunakamilisha uchimbaji wa kisima kipya chenye kina cha mita 180 kwenda chini. Kisima hiki kitatusaidia kujitegemea kwa maji yetu wenyewe bila kutegemea mtandao wa Dawasa,” amesema Kangurumjuli.

Amesema kukamilika kwa kisima hicho cha pili kutamaliza tatizo la uhaba wa maji katika stendi hiyo, huku akiwataka wafanyabiashara na wadau wengine kuwa na subira wakati jitihada hizo zikiendelea.

Kwa upande wao, wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wamesema tatizo hilo linahitaji ufumbuzi wa haraka kutokana na umuhimu wa huduma ya maji katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za usafirishaji.

“Shida ya maji hapa ni kubwa sana. Fikiria tangu Desemba 2025 hadi leo maji ya tumepata mara mbili pekee. Mara nyingi tunategemea maji yanayoletwa na maboza, lakini yanachelewa na mahitaji yanakuwa makubwa,” amesema mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaja jina lake.

Amesema shida hiyo kupata maji ya Dawasa ni tatizo kwa muda mrefu lakini viongozi waliopo wanaogopa kueleza kero hiyo, huku wakisema mradi huo ni mkubwa inakuaje hakuna miundominu hiyo.

“Shida ya maji hapa ni kubwa viongozi wanategemea maji ya maboza sasa ugumu unakuja pale ambapo huduma hiyo imechelewa kuletwa na watu wanahitaji,” amesema.

Meneja wa Stendi ya Magufuli, Isaac Kasebo amekiri kuwapo kwa changamoto ya upatikanaji wa maji katika kituo hicho, akisema huduma ya maji ilikuwa ikikatika kutokana na kutopata maji ya Dawasa mara kwa mara.

Kasebo amesema uongozi wa stendi ulilazimika kununua maji ya boza ili kukabiliana na upungufu huo na kusaidia kisima kilichopo ambacho hakikuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya matumizi ya kituo.

“Tulikuwa tunanunua maji ya boza ili kuongezea nguvu kisima cha maji kilichopo, ambacho hakikuwa na uwezo wa kuendana na mahitaji ya matumizi ya kituo,” amesema Kasebo.

Amesema hatua hiyo ilikuwa ya muda, huku akisema hawajawahi kukosa maji kwa zaidi ya saa moja, walikuwa wakichukua hatua mara moja pindi kiwango cha maji kinapopungua.

“Tunaelewa changamoto iliyopo, lakini hatuwezi kukaa kuona wananchi wanakosa huduma kwa sababu ya ukosefu wa maji. Halmashauri ilitoa fedha kwa ajili ya kununua maji hayo,” amesema.

Kasebo amesema ili kupata suluhisho la kudumu, uongozi wa stendi kwa kushirikiana na halmashauri wameanza mchakato wa kuchimba kisima kingine cha maji, sambamba na kile kilichopo, ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika.

“Tunahitaji kituo kiwe na maji yake yenyewe badala ya kutegemea Dawasa. Tayari tuna kisima kimoja na sasa tunaongeza cha pili, mkandarasi anaendelea na kazi ya uchimbaji,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema atasimamia suala hilo ikiwamo kuzungumza na mkurugenzi kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa haraka na mkandarasi anamaliza kuchimba kisima.

“Kwa kuwa hali ya maji inaendelea kutengemaa kwa upande wa Dawasa tutasiamamia maji yafike pale, mradi wa standi ile Serikali imetumia fedha nyingi na upembuzi yakinifu ulifanyika lazima huduma zote ziwepo,”amesema.