Dar es Salaam. Wazee kutoka mikoa mbalimbali nchini wameazimia mambo manne, ikiwemo kutaka mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uanze ili kujenga na kuimarisha umoja na amani katika Taifa.
Mengine ni pamoja na Serikali kutoa taarifa kamili, ndani ya muda muafaka na kwa uwazi, kuhusu vifo na mali zilizoharibiwa wakati wa maandamano yaliyoibua vurugu Oktoba 29, mwaka jana.
Pia, Serikali iendelee kusimamia haki na usawa wa raia, ikiwemo kuendelea kuwaachia wafungwa na mahabusu waliokamatwa kisiasa kupitia taratibu za kisheria.
Aidha, wazee hao wameazimia pia Tume ya Maridhiano itakayoundwa iwe na uwakilishi wenye mawanda mapana ya wajumbe wenye hekima, uadilifu na uzalendo usio na shaka.
Maazimio hayo yamesomwa leo, Alhamisi, Januari 22, 2026, na Mratibu wa Programu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Dk Musuto Chirangi, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo, Joseph Butiku.
Katika mkutano huo uliopewa jina la ‘Mkutano wa wazee wa kuimarisha haki, umoja na amani kwa Watanzania’, ulijadili mada nne za maafa na uharibifu wa Oktoba 29, mabadiliko ya Katiba, uzalendo, haki na uwajibikaji, pamoja na ujenzi wa amani, utatuzi wa migogoro na maridhiano.
Akifafanua kuhusu hoja hizo, Dk Chirangi amesema wanaunga mkono mchakato wa Katiba mpya uanze upya, uwe jumuishi, huru na wazi wa mabadiliko ya Katiba, ukihusisha vyama vyote na makundi mbalimbali ya wananchi.
“Mchakato uwe na ratiba itakayohitimishwa kwa kura ya maoni ya wananchi.
“Kuna pendekezo la kutofautisha na kutenganisha mamlaka na shughuli za Serikali dhidi ya vyama vya siasa. Wananchi wote tushiriki kikamilifu, maana Katiba ndiyo sheria mama na dira ya namna tunavyotaka kuishi na kujiongoza,” amesema.
Dk Chirangi amesema pia wazee wametoa pole kutokana na maafa na uharibifu uliotokeza Oktoba 29, huku wakiwataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu na wenye subira wakati tume ya kuchunguza matukio hayo, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiendelea kutekeleza majukumu yake.
“Serikali itoe taarifa kamili, ndani ya muda muafaka na kwa uwazi, kuhusu vifo na mali zilizoharibiwa. Baada ya kupata taarifa kamili, Serikali inaweza kuandaa pole (ubani) kwa waliofiwa na kutoa misaada ya kiafya na kisaikolojia kwa wahusika wote.
“Hatua stahiki zichukuliwe kwa wale watakaobainika kuvunja sheria kupitia vyombo vya kutoa haki,” amesema Dk Chirangi.
Kuhusu uzalendo, haki na uwajibikaji, Dk Chirangi amesema wazee hao wameazimia kila Mtanzania atangulize masilahi ya Taifa juu ya ubinafsi, uchama au makundi yoyote.
“Viongozi wawajibike kwa matendo yao, kuwe na uwazi wa rasilimali na mifumo madhubuti ya usimamizi na udhibiti inayofanya kazi ipasavyo.
“Hakuna aliye juu ya sheria, hivyo sote tusimamie utii wa sheria. Tutetee haki bila kuvunja sheria, tusimamie usalama pasipo kuvunja sheria, tulinde amani bila kuuza haki, na waliokamatwa kwa makosa ya kisiasa waachiwe,” amesema.
Pia, Dk Chirangi amesema Tanzania inakabiliwa na tatizo la ajira na kipato kidogo, hususan kwa vijana, hivyo wazee kama wazazi wa vijana hao wana wajibu wa kuwalea katika njia zinazofaa na kuishauri Serikali namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Tunasihi kuwa na busara katika uwasilishaji wa kero na kamwe tusikubali kushawishika kutengeneza mazingira ya nchi kutotawalika, maana uzoefu umeonesha madhara yake ni mabaya zaidi,” amesema na kuongeza;
“Wazee tunaamini Watanzania hatujapoteza uwezo wa kutambua changamoto zetu, wala hatujapoteza uwezo wa kuzungumza kwa uhuru, utulivu, kuaminiana na umoja kutatua kero zinazotukabili.”
Amesema wanasistiza umuhimu wa kusikiliza malalamiko kwa kufanya mazungumzo, kutatua migogoro na kutumia taratibu za usuluhishi wa kweli kuliko maandamano ya vurugu au yasiyokoma.
“Tunapendekeza kuwa, Tume ya Maridhiano itakapoundwa, iwe na uwakilishi wenye mawanda mapana ya wajumbe wenye hekima, uadilifu na uzalendo usio na shaka. Pia, iongozwe na raia anayestahiki, asiyehusika kuongoza upande wowote wa kisiasa.
“Maelezo ya kutosha yawepo wazi kueleza aina ya maridhiano na wahusika. Kila mtu ajiepushe na akemee matamko na vitendo vya kibaguzi au vinavyohamasisha ubaguzi wowote,” amesema.
Mbali na hilo, Dk Chirangi amesema wazee hao wametoa wito kwa Watanzania wote kuwajibika na kuwawajibisha wasiowajibika kwa mujibu wa Katiba, sheria na kanuni zinazoongoza.
Baada ya Dk Chirangi kusoma maazimio hayo, Butiku amesema imani yao ni kwamba mambo hayo yatasaidia Taifa, na hata washiriki yatawasaidia wanapokwenda.
“Vikao vya wazee si vya kuandaliwa na taasisi pekee. Naishukuru Serikali, tumezungumza kwa uhuru. Tunamshukuru Rais Samia. Kwenye wazee, hakuna linaloharibika,” amesema Butiku.