Afya bora inaanzia kwenye sahani mezani

Unataka kuwa na afya njema, ngozi yenye mvuto, rangi nzuri na mwonekano unaovutia? Hujachelewa. Jibu la maswali haya yote linaanzia kwenye lishe, kwani lishe ndiyo msingi mkuu wa afya ya binadamu.

Mwananchi imezungumza na wataalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) ili kufahamu kwa undani maana ya lishe bora inayoimarisha kinga ya mwili na mambo muhimu ambayo jamii inapaswa kuyazingatia.

Fatma Juma na Nusura Lulengelule, ambao ni maofisa lishe watafiti kutoka TFNC, wanaeleza kuwa lishe ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyokitumia chakula. Hatua hizo ni pamoja na ulaji wa chakula, usagaji, umeng’enyaji, ufyonzwaji wa virutubishi na matumizi yake mwilini. Kwa ujumla, lishe hugawanyika katika makundi mawili makuu ambayo ni lishe bora na lishe duni.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, lishe bora ni hali inayotokana na kula mlo kamili unaokidhi mahitaji ya mwili, ukiwa na mchanganyiko wa vyakula kutoka katika makundi yote muhimu ya chakula, sambamba na kufanya mazoezi ya mwili. Lishe bora husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuuwezesha mwili kupambana na magonjwa mbalimbali.

Kwa upande mwingine, lishe duni ni hali ambapo mwili haupati virutubishi vinavyokidhi mahitaji yake, ama kutokana na kula chakula kisichokidhi mahitaji ya lishe au uwepo wa maradhi.

Fatma  anaeleza kuwa lishe bora huimarisha kinga ya mwili kwa kuupa mwili virutubishi muhimu vinavyohitajika katika utekelezaji wa kazi zake za kila siku.

Anafafanua kuwa virutubishi ni viini lishe vilivyomo kwenye chakula, ambavyo huuwezesha mwili kuzalisha nguvu, kujenga na kulinda mwili dhidi ya magonjwa.

Anaongeza kuwa vyakula vyote huwa na zaidi ya aina moja ya kirutubishi, ingawa hutofautiana kwa kiasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi maalumu mwilini, na mara nyingi virutubishi hutegemeana ili kufanya kazi kwa ufanisi. Mwili wa binadamu huhitaji virutubishi vikuu ambavyo ni wanga, protini, mafuta, vitamini na madini.

Fatma anabainisha kuwa kinga ya mwili ni ngao ya asili inayoulinda mwili dhidi ya magonjwa na maambukizi. Anasisitiza kuwa hakuna chakula kimoja pekee kinachoweza kuzuia magonjwa yote, bali mwili huhitaji mchanganyiko wa vyakula mbalimbali vyenye virutubishi tofauti ili kuimarisha mfumo wa kinga kwa ufanisi.

Anasema: ‘’ Vyakula vinapaswa kuliwa kwa mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula. Kundi la nafaka, mizizi yenye wanga na ndizi mbichi hutoa nishati ya kutosha kwa ajili ya kuupatia mwili nguvu.’’

Kundi la mbogamboga linajumuisha mboga za majani na zile zisizo za majani. Mboga hizi zina vitamini na madini yanayosaidia kulinda mwili dhidi ya maradhi na kuuwezesha mwili kufanya kazi zake vizuri.

Kundi la matunda linahusisha matunda ya aina zote, yakiwemo ya porini na yale ya kawaida, ambayo hutoa vitamini muhimu kwa ajili ya kuimarisha kinga ya mwili.

Kundi la jamii ya kunde, karanga na mbegu zenye mafuta hujumuisha vyakula kama maharagwe, dengu, njegere, soya, njugu mawe, mbaazi, choroko, kweme na fiwi. Vyakula hivi vina protini nyingi zinazosaidia kujenga mwili, kukarabati seli zilizochakaa, kuimarisha kinga ya mwili na kusaidia usafirishaji wa virutubishi mwilini.

Kundi la vyakula vyenye asili ya wanyama linajumuisha nyama, samaki, dagaa, maziwa, mayai, jibini, maini, figo, pamoja na wadudu wanaoliwa kama senene na nzige.

Madhara ya kutozingatia lishe bora

Nusura  anaeleza kuwa ulaji usiofaa, kama kutumia vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi na sukari nyingi, pamoja na kula mlo usio na mchanganyiko wa makundi ya chakula kulingana na mahitaji ya mwili, huongeza hatari ya kupata madhara mbalimbali ikiwamo njaa iliyojificha.

Hali hii husababisha upungufu wa vitamini na madini muhimu mwilini, kushuka kwa kinga ya mwili, upungufu wa damu, uoni hafifu, pamoja na kuathiri ukuaji na maendeleo ya mwili, hasa kwa watoto.

Aidha, ulaji usiozingatia mahitaji ya mwili unaweza kusababisha uzito mkubwa, uzito uliokithiri au kiribatumbo kutokana na kuhifadhiwa kwa ziada ya chakula kama mafuta mwilini. Kwa upande mwingine, kula chakula kidogo kisichokidhi mahitaji ya mwili husababisha uzito pungufu na ukondefu.

Lulengelule anashauri jamii kula mlo kamili unaojumuisha makundi yote ya chakula kila siku kulingana na mahitaji ya mwili. Kula vyakula mchanganyiko hutoa virutubishi mbalimbali vinavyosaidiana katika utendaji wa kazi za mwili.