Bunge jipya litaleta chochote kipya kwa wastaafu?

Bunge jipya limeanza kazi Januari hii ya mwaka huu wa 2026, likitegemewa kufanya mambo mengi mapya ili kuiendeleza nchi yetu. Linategemewa kufanya hivyo kwa miaka mitano ijayo, ambapo wale watakaoonekana wametenda vyema kuiendeleza nchi watapewa na wananchi miaka mingine mitano ya kufanya vitu vyao vya kuendeleza nchi.

Lakini wale “wenzangu mimi” ambao wataonekana hawakufanya lolote lenye mwelekeo wa kuiendeleza nchi, zaidi ya kushangilia kwa kugonga viti, watatakiwa wachape lapa tu fasta, na kutuachia nchi yetu, na wawakilishi wetu waendelee kutuwakilisha kutafuna mema ya nchi, kama vile wengine hatuna magego!

Bila unafiki wowote, mstaafu wetu anasema wazi kuwa hategemei lolote jipya kutoka kwa wawakilishi wetu linalowahusu wastaafu wa kima cha chini. Litoke wapi? Mstaafu anajulikana kuwa bado yupo nchi hii? Wawakilishi wameishamzungumzia mara ngapi kwenye lile Bunge la zamani? Hajaenda Burundi tu?

Mstaafu alianza kukata tamaa alipoona kuna wawakilishi wachache waliochaguliwa na wananchi kwenye uchaguzi wenye miaka 70 na kuendelea, yaani wazee, waliochaguliwa kuingia kwenye hilo Bunge jipya kuwazungumzia wastaafu na wazee kwa ujumla.

Inawezekana wastaafu na wazee hawakuwa na nguvu ya kupita huku na huko kuwaomba kura wananchi ili wakawasemee wazee yanayowahusu, kama lile la matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi, ambalo limeishia kuwa maneno ya kanga, tena kanga rejekti!

Mstaafu wetu alitegemea japo nafasi mbili za wabunge wa kuteuliwa ziachiwe wastaafu walioijenga nchi hii, waseme yanayowasibu. Haikuwa. Hakuna anayetaka kusikia kelele za wazee au nyongeza ya pensheni. Kuhamia Burundi kunawatosha!

Kwa masikitiko, mstaafu wetu anakumbuka kuwa miaka 10 ya Bunge lililopita hakuna wabunge waliopambana kisawasawa mstaafu aongezwe pensheni yake ya shilingi laki moja na elfu tano aliyokuwa akipokea kwa mwezi kwa miaka… mama wee!… ishirini!

Mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga nchi hii?

Wawakilishi wetu walikuwa bize kupitisha fasta muswada wa kuwalipa pensheni inayoeleweka wenza wa waheshimiwa wastaafu, mbali ya wawakilishi hao kuwa bize kujiongeza mishahara… ambapo mpaka wanaondoka mwishoni mwa mwaka jana walikuwa wanapokea kwa mwezi shilingi… mama wee!… milioni kumi na nne kwa mwezi, huku mstaafu aliyeijenga nchi hii akipokea shilingi… Mungu wangu!… laki moja na elfu hamsini!

Suala la kuwakumbuka wenza wa wastaafu wapewe japo shilingi elfu ishirini kwa mwezi halikupata kuingia vichwani mwao wawakilishi wa Bunge la miaka kumi iliyopita, pamoja na kwamba huyu mwenza ndiye aliyemfanya mstaafu kuwa imara kuijenga nchi hii kwa msosi, kumfulia na kumpigia pasi mstaafu.

Yaani, mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga nchi hii anapokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka ishirini, na hakuna hata mtu japo anayekohoa tu! Na watu wako bize kupiga makofi meza kushangilia hoja, badala ya kuzaba makofi wale wote wanaohusika na nyongeza ya pensheni ya wastaafu, mwe!

Hawa ndio walikuwa wawakilishi wa Bunge lililopita ambao kwa kazi ngumu ya kushangilia hoja kwa miaka mitano tu walipata kiinua mgongo cha shilingi… mama wee!… milioni mia tatu na…

Yule mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga kweli nchi kwa jasho na damu yake kwa miaka 40, rudia hapo, miaka arobaini alipata kiinua mgongo cha tushilingi milioni 30, na sasa anapata pensheni ya shilingi laki moja na elfu hamsini! Wawakilishi wa Bunge jipya waanzie hapa penye hesabu rahisi tu!

0754 340606 / 0784 340606