Magonjwa  yasiyoambukiza yanavyowanyemelea vijana | Mwananchi

Arusha. Magonjwa ya moyo ambayo kwa muda mrefu yalionekana kuwa ni tatizo linalowakumba zaidi wazee, sasa yameanza kuwakumba vijana kwa kasi inayoongezeka.

Mabadiliko haya yamezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wataalamu wa afya, huku yakionesha wazi kuwa mtazamo wa awali kuhusu magonjwa hayo haupo tena.

Zamani, haikuwa jambo la kushangaza kumkuta mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea akiwa na ugonjwa wa moyo, hali iliyochangiwa zaidi na kupungua kwa nguvu za mwili, kutojihusisha na mazoezi ya mara kwa mara pamoja na kudhoofika kwa baadhi ya viungo vya mwili.

Watalaamu wanaeleza kuwa, isipokuwa kwa watoto wachache wanaozaliwa na matatizo ya moyo, vijana hawakuwa kundi linalotarajiwa kuathirika kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, hali hiyo imeanza kubadilika kwa kasi kutokana na mitindo mibaya ya maisha inayoendelea kushika kasi miongoni mwa vijana, hali inayogeuka kuwa mwiba mkubwa kwa afya ya moyo na ustawi wa nguvu kazi ya taifa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter  Kisenge, anasema magonjwa ya moyo pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla,  yanaongezeka kwa kasi kubwa duniani kote.

Anabainisha kuwa zaidi ya watu milioni 20 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, na kati ya hao, asilimia 32 ya vifo vinatokana na magonjwa ya moyo.

Kwa mujibu wa Dk Kisenge, takwimu hizo ni ishara tosha kuwa tatizo hilo si dogo wala la kupuuzwa, hasa linapoanza kuathiri vijana ambao ndio nguzo ya maendeleo ya taifa.

Anasema kupitia ufadhili wa Rais Samia Suluhu Hassan, JKCI imeendesha kambi za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika zaidi ya mikoa 23 nchini.

Katika safari hizo, taasisi imefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 24,000 waliopimwa afya ya moyo. Matokeo ya uchunguzi huo yamekuwa ya kushangaza, baada ya zaidi ya asilimia tisa ya waliopimwa kubainika kuwa na matatizo ya moyo, huku asilimia tano kati yao wakiwa vijana.

“Cha kushangaza zaidi ni kwamba hatutarajii kuona vijana wa umri wa miaka 20 hadi 40 wakiwa na magonjwa ya moyo. Huu ni umri ambao kwa kawaida mtu anapaswa kuwa na afya njema na nguvu nyingi,” anasema.

Anaongeza kuwa hali halisi iliyoonekana katika kambi hizo imeonesha kuwa vijana wengi waliokutwa na matatizo ya moyo, walikuwa tayari wameathirika kwa kiwango kinachohitaji ufuatiliaji wa karibu au hata rufaa ya matibabu ya kibingwa.

Mtindo wa maisha adui mkubwa

Kwa mujibu wa Dk Kisenge, mtindo mbaya wa maisha ndio chanzo kikuu cha ongezeko la magonjwa ya moyo miongoni mwa vijana.

Anataja uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, matumizi ya bangi na shisha, kutofanya mazoezi, ulaji usiozingatia lishe bora pamoja na unene uliopitiliza kuwa sababu zinazoongoza.

Anasema unywaji wa pombe kupita kiasi hauhusu tu kunywa chupa chache mara chache, bali ni pale vijana wanapokunywa pombe nyingi au kali mara kwa mara. Pombe nyingi huathiri misuli ya moyo na kufanya ishindwe kusinyaa kwa nguvu inayotakiwa, hali inayoweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi zake ipasavyo.

Mbali na pombe, anataja pia uvutaji wa sigara, bangi na shisha kuwa kichocheo kikubwa cha magonjwa ya moyo. Moshi wa bidhaa hizo huathiri mishipa ya damu, huongeza hatari ya shinikizo la damu, mshtuko wa moyo na kiharusi, na wakati mwingine husababisha vifo vya ghafla miongoni mwa vijana.

Maisha ya kukaa na kutembea kidogo

Mabadiliko ya maisha ya kisasa yamechangia kwa kiasi kikubwa pia ongezeko la magonjwa ya moyo kwa vijana. Dk Kisenge anasema vijana wengi wameacha kutembea kwa miguu hata kwa umbali mfupi, badala yake wanategemea usafiri wa bodaboda, teksi au magari binafsi.

Anasema hali hiyo inaufanya mwili ushindwe kufanya kazi ipasavyo, kwani haupati nafasi ya kuchoma mafuta na kutoa jasho.

Kutofanya mazoezi kunachangia kuongezeka kwa mafuta mwilini, shinikizo la damu na kisukari, magonjwa ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na afya ya moyo. Anawahimiza vijana kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki.

Lishe imeendelea kuwa changamoto kubwa kwa vijana wa kizazi cha sasa. Dk Kisenge anasema vijana wengi wanakula vyakula vyenye wanga na mafuta mengi bila kufanya mazoezi ya kutosha, huku wengine wakila chakula kizito nyakati za usiku muda mfupi kabla ya kulala.

Anasema tabia hiyo husababisha mwili kuhifadhi chakula hicho kama mafuta, na mafuta yanapozidi huathiri mishipa ya damu na kuusababishia moyo mzigo mkubwa.

Hali hiyo pia huchangia kuibuka kwa magonjwa mengine yasiyoambukiza kama kisukari, ambayo nayo yameonekana kuongezeka miongoni mwa vijana waliopimwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Dk Kisenge anawahimiza vijana kujitokeza kupima afya zao mara kwa mara kupitia kampeni ya “Jua namba zako”.

Kampeni hiyo inalenga kuwafanya wananchi, hususan vijana, kufahamu viashiria muhimu vya afya zao ikiwemo shinikizo la damu, uzito, kiwango cha sukari na mafuta mwilini.

Anasema upimaji wa mara kwa mara husaidia kugundua matatizo mapema na kuchukua hatua kabla madhara hayajawa makubwa.

Kwa upande wake, kijana Saimon Lemomo, mkazi wa Arusha, anasema changamoto za maisha, ukosefu wa ajira na shinikizo la kijamii vimekuwa vikichangia vijana wengi kujiingiza katika mitindo mibaya ya maisha.

‘’Baadhi ya vijana hutumia pombe, sigara na shisha kama njia ya kujituliza kisaikolojia kutokana na mawazo na changamoto wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku, bila kufahamu athari zake za muda mrefu kwa afya zao,’’ anaeleza.