Dondoo muhimu za afya kwa wanawake miaka 40+

Wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea wako katika hatari ya kuathiriwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Changamoto hizi ni pamoja na saratani, uvimbe usio wa saratani, pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari, ongezeko la lehemu mwilini na unene uliokithiri.

Vilevile, kundi hili lipo katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kama VVU, kifua kikuu, malaria, maambukizi ya njia ya mkojo pamoja na magonjwa ya zinaa yanayoathiri viungo vya uzazi.

Aidha, kuna changamoto za kiafya zinazoambatana na ukomo wa hedhi, ikiwamo udhaifu wa mifupa, kuongezeka kwa uzito na matatizo ya afya ya akili. Kadri umri unavyoongezeka, kinga ya mwili hupungua, hali inayoongeza uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa mbalimbali.

Zifuatazo ni dondoo muhimu za kiafya zitakazosaidia wanawake waliopo katika umri huu kupunguza hatari ya magonjwa na kuishi maisha bora na yenye afya kwa muda mrefu.

Zingatia lishe bora
Epuka ulaji holela. Punguza matumizi ya chumvi, sukari, mafuta na vyakula vyenye wanga mwingi. Pendelea kula mboga za majani, matunda, nafaka zisizokobolewa, pamoja na protini zinazotokana na samaki na jamii ya kunde. Hakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku.

Fanya mazoezi ya mwili mara kwa mara
Jishughulishe na mazoezi mepesi au shughuli za kila siku zinazouhusisha mwili kama kazi za nyumbani au bustani. Kutembea kwa muda wa kutosha kila siku husaidia kuimarisha afya ya mwili na akili.

Pata uchunguzi wa kiafya wa mara kwa mara
Ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, angalau mara moja au zaidi kwa mwaka kulingana na ushauri wa wataalamu wa afya. Shiriki katika kampeni za kitaifa za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti, na hakikisha unapokea chanjo zote muhimu.

Fuata matibabu kikamilifu
Wanawake wanaoishi na magonjwa sugu kama VVU, shinikizo la damu, kisukari, saratani au matatizo ya afya ya akili wanapaswa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kufuata matibabu kikamilifu bila kukatisha.

Epuka matibabu yasiyo rasmi
Epuka kutumia dawa au tiba zinazotangazwa mitandaoni au mitaani bila ushauri wa mtaalamu wa afya. Hii ni pamoja na matumizi holela ya dawa za kutibu ugumba, maambukizi sugu ya njia ya uzazi, dawa za kupunguza uzito au vipodozi vilivyopigwa marufuku vinavyobadili rangi ya ngozi.

Linda afya ya akiliĀ  na uhusiano
Hakikisha unakuwa na mahusiano mazuri kifamilia na kijamii. Migogoro ya mahusiano huongeza hatari ya matatizo ya afya ya akili, hususan sonona, ambayo wanawake wa umri huu wako katika hatari kubwa ya kuipata. Afya ya akili ikidorora, kinga ya mwili hushuka na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa mengine.
Pia, fanya ibada, tafakari na mazoezi ya kupunguza msongo wa mawazo kama yoga au mbinu za kupumua.

Pumzika na pata usingizi wa kutosha
Hakikisha unapata usingizi wa kutosha kila usiku. Ikiwa unakabiliwa na changamoto ya kukosa usingizi au usingizi unaokatika mara kwa mara, wahi kituo cha afya mapema kwa ushauri na matibabu.

Ongeza uelewa wa masuala ya afya
Jiongezee maarifa kuhusu changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili wanawake. Elimu ya afya hukuwezesha kuchukua hatua za kinga mapema kabla ya matatizo kujitokeza.

Pata ushauri wa kitaalamu wakati wa ukomo wa hedhi
Iwapo umefikia au unaelekea kufikia ukomo wa hedhi, muone daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kwa ushauri unaoendana na hali yako, kwani kipindi hiki huambatana na changamoto mbalimbali za kiafya.

Jiwekee kinga ya kifedha na kiafya
Tambua kuwa mwanamke ni kundi maalum katika jamii. Kuwa na bima ya afya, zingatia njia zote za kujikinga na magonjwa ikiwamo kuwa na mpenzi mmoja na kutumia njia salama za kujamiiana. Aidha, zingatia mtindo bora wa maisha kwa kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku, kudumisha usafi wa mwili, pamoja na kutunza mazingira unayoishi.