Mali ni mtihani kwako, unaitafutaje? | Mwananchi

Haifichiki kwa mtu mwenye akili timamu kuwa Sharia ya Allah imekuja kulinda na kutimiza masilahi ya waja, na kuwalinda na maafa, ufisadi, na kuvunjika kwa mpangilio wa jamii. Wanazuoni wa Kiislamu wamekubaliana kuwa kulinda mali, kwa ujumla wake, ni miongoni mwa misingi mikuu ya Sharia.

Ama yanayohusiana na kuitafuta mali, kuikuza na kuitumia, hayo yako katika kiwango cha mahitaji muhimu (ḥajiyyaat) yanayopewa nafasi inayokaribia daraja la dharura.

Kwa sababu hiyo, kuzungumzia njia na mipaka ya kipato halali katika Uislamu si jambo la ziada au la pembeni, bali ni miongoni mwa wajibu muhimu unaopaswa kupewa uzito unaostahiki.

Hakika, kipato halali ni katika wajibu mkubwa kabisa, kama alivyosema Mtume (Rehema na amani ziwe juu yake) : “Kutafuta riziki halali ni wajibu juu ya kila Muislamu” Hasa katika zama hizi ambazo watu wengi hawajali tena iwapo wanachokipata ni halali au haramu.

Mtume wa Allah, alibashiri hali hii kwa kusema: Itawadia kwa watu zama ambazo mtu hatajali anachokipata; je, ni cha halali au cha haramu.”  Athari  ya kula haramu hujitokeza katika mienendo na tabia ya mtu, na hatimaye huathiri viungo vyake vyote.

Kwa sababu hiyo, ni bora kwa muumini kipato chake  kiwe cha halali, kuliko kuomba watu au kujipatia kipato cha haramu. Mtume wa  Allah amesema: Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake, mmoja wenu akichukua kamba yake akaenda mlimani akakata kuni, kisha akazibeba mgongoni mwake na akala (kwa kipato hicho), hilo ni bora kwake kuliko kuwaomba watu; na ni bora kwake kuliko kula haramu.” Na mla haramu hufungiwa milango ya mbinguni. Mtume  wa Allah alitaja habari ya mtu anayesafiri muda mrefu, mwenye nywele za timtim na zilizochafuka na vumbi, anainua mikono yake mbinguni akiomba: Ewe Mola wangu! Ewe Molawangu !” ilhali chakula chake ni cha haramu, kinywaji chake ni cha haramu, mavazi yake ni ya haramu, na amekuzwa kwa (kipato) haramu; basi vipi dua yake itakubaliwa mtu huyo?”

Uislamu umeipa mali uangalizi wa pekee na kuwa miongoni mwa mahitaji ya lazima ya maisha. Mara nyingi Qur’an imeunganisha kutajwa kwa mali na nafsi pamoja na watoto, ili kubainisha hadhi yake, kusisitiza umuhimu wake, na kuthibitisha kuwa Uislamu ni dini ya maisha. Mali ni nguzo ya kusimama kwa dini, kama ilivyo nguzo ya kusimama kwa miili, na ni sababu ya kuendelea kwa maisha.

Mali Ni uti wa mgongo wa maisha; kupitia mali hupatikana maslahi ya watu, ustawi wao, na kutimizwa kwa mahitaji yao. Mali pia ni pambo la maisha ya dunia. Mtu anapokuwa fakiri hudharauliwa na wengine, na dunia humbana licha ya upana wake.

Vivyo hivyo, hazina za taifa katika nchi zinapokauka, hadhi yake nchi hiyo huporomoka, adui huidharau, hushindwa kujilinda, na kuwa huru kimaamuzi.

Mali pia ni uwanja wa mitihani na majaribio; wapo wanaofanikiwa na kuokoka kupitia mali zao, na wapo wanaoharibika na kuangamia kwa sababu ya kumiliki mali.

Kwa sababu hiyo, Sharia ya Kiislamu imeeleza kwa kina njia halali za kuipata mali, namna ya kuizungusha na kuiwekeza, jinsi ya kuitumia na kunufaika nayo, na imeweka mipaka na kanuni zinazoainisha yaliyo halali na yaliyo haramu. Pamoja na hadhi na umuhimu wake wote, mali hubaki kuwa njia, si lengo. Lengo lake ni kusimamisha maisha, kutimiza mahitaji, na kutekeleza wajibu.

Allah amesema. “Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi.  (28:77). Na Mtume  wa Allah alimwambia Amr bin Al-Aṣ ( Allah Amridhie): “Ewe Amr! Mali iliyo bora ni inayomilikiwa na mtu mwema.”

Iwapo mali itageuzwa kuwa lengo la maisha, na ikamshughulisha mwanadamu mpaka akasahau au akapuuza yale yaliyofaradhishwa na Allah, basi hapo mali hubadilika na kuwa mzigo mzito, fitina, na chanzo cha maangamizi kwa mwenyewe.

Katika hali hiyo, mali huwa sababu ya hasara, kuporomoka, na maangamizi, badala ya kuwa chombo cha kheri na ujenzi wa maisha. Allah amesema. “Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema” (2:195)  

Kuna njia kuu za kujipatia mali, zipo njia za  kiasili kama vilekuajiriwa au kuajiri, biashara, ufugaji, kilimo,  viwanda au ufundi.

Njia hizi zote ni ziko katika hukmu ya uhalali kwa mujibu wa Jopo la wanazuoniwa Sharia ya Kiislamu.  Kadhalika zipo njia za halali zisizo za kudumu au za kawaida za kujipatia mali. Baadhi yake hupatikana bila malipo au mbadala, kama vile mirathi, zawadi, sadaka, mahari n.k.