Polisi yamshikilia mwenyekiti Chadema Mbeya Vijijini, yataja sababu

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mbeya Vijijini Getruda Lengesela kwa tuhuma mbalimbali za kijinai ikiwamo uchochezi.

Mtuhumiwa huyo anakamatwa ikiwa zimepita siku mbili tangu viongozi wengine wawili wa chama hicho, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa huo, Masaga Kaloli na Mwenyekiti wa Bavicha mkoani humo, Elisha Chonya kukamatwa na jeshi hilo kwa tuhuma kuhamasisha mkusanyiko isivyo halali.

Wawili hao walikamatwa Januari 21 katika Kijiji na Kata ya Inyala wakati Chadema ikijiandaa kuadhimisha miaka 33 ya kuzaliwa kwa Chama hicho, iliyokuwa imepangwa kuambatana na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo michezo na chakula ya pamoja.

Katika taarifa ya Jeshi la Polisi, ilieleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakifanya maandalizi na kuhamasisha watu kukusanyika kufanya mkutano bila kufuata taratibu za kisheria.

“Ikumbukwe Chadema imezuiliwa na mahakama kufanya shughuli zozote za kisiasa, upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 23 na Jeshi hilo, imesema mtuhumiwa amekamatwa Januari 22 saa 3:40 usiku katika eneo la Nsalala katika mji mdogo wa Mbalizi wilayani humo mkoani Mbeya.

“Anashikiliwa kwa tuhuma mbalimbali za za kijinai ikiwamo uchochezi, upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake” imesema taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoani humo.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Mbeya, Hamad Mbeyale amesema huu ni mwendelezo wa viongozi wao kushikiliwa, akieleza kuwa bado hawatakata tamaa kwa mazingira wanayopitia.

Amesema haki ina gharama na inahitaji uvumilivu, akieleza kuwa kwa sasa wanafuatilia kujua hatma ya kiongozi huyo na wengine walioshikiliwa siku mbili zilizopita ili kuachiliwa huru.

“Niwaombe wananchi kuendelea kuvumilia, tunapitia vipindi vigumu ila ndio njia ya kuelekea kupata haki, gharama, muda na uvumilivu ni muhimu sana kwa wakati huu tunapolipambania Taifa” amesema Mbeyale.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikiliwa watuhumiwa watatu Mseven Menat, Fred Lulandala na Joseph Ngelenge kwa tuhuma za kusafirisha dawa zakulevya aina ya bhangi kilo 168.

Watuhumiwa hao walikamatwa Januari 21katika stendi kuu ya mabasi jijini Mbeya wakiwa kwenye bajaji, huku dawa hizo zikiwa zimepakiwa kwenye mabegi nane wakitaka kuzisafirisha kwenda mkoani Arusha.

“Watuhumiwa wameeleza kuingiza nchini dawa hizo kutoka nchi jirani na walitaka kuzisafirisha kwa njia ya basi kuelekea Arusha, upelelezi unakamilishwa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa,” imeeleza taarifa ya polisi.