Stand Utd yabadili gia, nyota 10 wakimbia njaa

SUALA la ukata limeendelea kuitesa Stand United ya Shinyanga na dirisha dogo zaidi ya wachezaji 10 wameondoka na wengine kugoma.

Hali hiyo imelilazimisha benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo kuja na mbinu mbadala za kupata wachezaji watakaokubali kucheza kwenye mazingira magumu yasiyo na uhakika wa kupata stahiki mwisho wa mwezi.

Timu hiyo iko nafasi ya 11 kwenye Ligi ya Championship ikiwa na alama 14 baada ya michezo 15, huku ikishinda mitano, sare mbili na kupoteza nane na imefunga mabao 11 na kuruhusu 19.

Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Stand United, Feisal Hau wachezaji zaidi ya 10 akiwemo Raymond Masota aliyetimkia Geita Gold, Amri Msenda, Paschal Wagana na Abel Hegela wameondoka na wengine wakitokomea bila kuaga kutokana na kutopata stahiki zao.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa klabu umelitaka benchi la ufundi linapotafuta wachezaji wapya idadi isivuke 21, huku makocha wakihitaji wachezaji 25 ili kuwa na uhakika wa kufanya vizuri mzunguko wa lala salama.

“Tunaendelea kuchagua wachezaji na kufanya nao mazungumzo kwasababu hali ilivyo tunatumia ushawishi wetu kama makocha tu na kuwaomba waje wacheze kwa sharti wakipata timu ya kuwapa mshahara basi wanaondoka bure,” amesema Hau na kuongeza;

“Tumeona kuna wachezaji wengine wazawa wa Shinyanga ina maana wakipewa nafasi wanaweza kusaidia, wasiwe na gharama na wakaelewa kazi yetu, baadhi tumeshazungumza nao na wamecheza mechi yetu ya kirafiki na Pamba tunaamini watatusaidia.”

Amesema katika usajili huo wanaangalia zaidi eneo la ulinzi na ushambuliaji kwani ndiyo yaliyoathirika zaidi kwa wachezaji kuondoka, huku akiwa na matumaini endapo wachezaji wapya watajitoa basi timu hiyo itamaliza katika nafasi nzuri na kukwepa kushuka daraja.

“Kama tumeweza kusogea tukafika hapa raundi ya pili tutakuwa bora zaidi, tunaamini kutokana na ushawishi tunaondelea kufanya kwa wachezaji tunaofahamiana nao na wale wazawa wa hapa Shinyanga basi tutafanya vizuri kwani baadhi yao tumeshakuwa na uhakika nao,” amesema.