WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo kwa watendaji wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokozi cha Kikanda – Mwanza, chenye thamani ya takribani shilingi bilioni 19.8, kuhakikisha kituo hicho kinaendeshwa kwa saa 24 na kwa ufanisi wa hali ya juu.
Amesema hayo leo Januari 23, 2026 baada ya kutembelea kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokozi, jijini Mwanza
Amesisitiza kuwa huduma za uokozi ni kazi ya kuokoa maisha, hivyo hakuna uvumilivu kwa uzembe, kuchelewesha utoaji wa huduma za msaada pindi inapohitajika.
“Hii ni kazi ya kuokoa maisha. Uzembe, kusinzia au kuchelewesha kutoa msaada ni kuhatarisha maisha ya Watanzania. Kituo hiki lazima kifanye kazi saa 24.”
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema ujenzi wa kituo hicho ni uthubitisho wa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwatumikia watanzania na kujali changamoto mbalimbali nchini.
“Kituo hiki kilikuwa kijengwe mwaka 2018 kwenda Mwaka 2020, kilisimama baada ya wenzetu kujitoa, lakini Rais Dkt. Samia akasema tutakijenga kituo hiki kwa fedha zetu ili wavuvi waweze kupata huduma ya usalama katika kazi zao”.

.jpeg)
.jpeg)
