Straika Transit Camp haamini alichofanya Championship

MSHAMBULIAJI wa Transit Camp, Adam Uledi amesema tangu amecheza mpira wa miguu hajawahi kufunga idadi kubwa ya mabao 11, aliyoyafunga msimu huu, jambo linalompa matumaini makubwa ya kuendelea kupambana ili azidi kuonekana zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Uledi anayeongoza kwa mabao msimu huu baada ya kufunga 11 kati ya 21 yaliyofungwa na kikosi hicho msimu huu, amesema kuaminiwa na benchi la ufundi na ushirikiano na wenzake ndio sababu kubwa ya kufanya vizuri.

“Naamini Transit ni timu inayoweza kunirudisha tena katika nafasi ya kuonekana zaidi kwa sababu nilianza kupotea baada ya changamoto za hapa na pale, nashukuru sana benchi la ufundi kwa kuendelea kuniamini na sitawaangusha,” amesema Uledi.

Nyota huyo amejiunga na kikosi hicho msimu huu, baada ya kuachana na Stand United ‘Chama la Wana’ ya mkoani Shinyanga, huku akizichezea pia Namungo, Ruvu Shooting, African Sports, Coastal Union, TMA, KenGold na timu ya vijana ya Yanga.

Katika kipindi cha miezi sita aliyoichezea Stand aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025, akitokea KenGold, nyota huyo alifunga mabao matatu, ingawa hadi sasa zikiwa zimechezwa raundi 15 tu, tayari ameifungia Transit Camp mabao 11.

Katika mechi hizo 15 ilizocheza Transit Camp hadi sasa msimu huu, imeshinda 10, ikitoka sare mitatu na kupoteza miwili tu na kikosi hicho kimefunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12, kikiwa nafasi ya nne na pointi 33.