TANZANIA Prisons imekamilisha usajili wa washambuliaji George Mpole na Emmanuel Martin, na tayari wamejiunga kambini kujiandaa na mechi dhidi ya JKT Tanzania itakayopigwa kesho, Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Taarifa za ndani kutoka timu hiyo zimedai usajili wa Mpole ambaye aliyeifungia mabao mawili Pamba Jiji kabla ya kuachana nayo msimu uliyopita na Martin aliyetokea Dodoma Jiji, utaongeza nguvu kubwa eneo la ushambuliaji.
Mechi nane ilizocheza Prisons, imeshinda mbili, sare moja, imefungwa tano, mabao ya kufunga matatu ya kufungwa sita, imekusanya pointi saba, inakwenda kukutana na JKT Tanzania inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi 12, imeshinda mechi tatu, sare tatu, imefungwa mbili,inamiliki mabao saba, imeruhusu mabao saba, imecheza mechi nane.
“Ujio wa Mpole aliyewahi kuibuka kinara wa mabao 17 msimu wa 2021/22 akiwa Geita Gold na Martin aliyewahi kuichezea Yanga 2015/16 ni ongezeko la mabao katika timu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Pia tunaendelea kufanya mazungumzo na beki Gustavo Saimon aliyeichezea Coastal Union msimu uliyopita, ili kuongeza nguvu eneo la ulinzi ili timu iwe imara kila eneo.”