Tanga. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB), Deogratius Kuyukwa amesema benki hiyo inatumia kikamilifu maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kuwafikia wananchi wenye biashara pamoja na wale wanaotarajia kuanzisha biashara, kwa lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji wa mitaji.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yanayoendelea kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026 mkoani Tanga, Kuyukwa amesema wiki hiyo imekuwa fursa muhimu kwa TIB kukutana moja kwa moja na wajasiriamali, kusikiliza changamoto zao na kutoa suluhisho linaloendana na mahitaji yao ya kifedha.
Amesema maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yameshirikisha taasisi mbalimbali za kifedha kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Tanga, hali iliyowezesha wananchi kupata uelewa mpana kuhusu huduma za kifedha, mikopo, bima pamoja na masuala ya usimamizi wa fedha.
Kwa mujibu wa Kuyukwa, TIB kama benki ya maendeleo imejikita zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ufadhili wa miradi ya maendeleo kupitia mikopo ya muda mrefu na muda mfupi, hususan katika sekta za kilimo, viwanda, miundombinu na huduma.
“Kupitia Wiki ya Huduma za Fedha, sisi kama Benki ya Maendeleo tumekuja kuwajengea wananchi uelewa wa huduma tunazotoa, ikiwemo ufadhili wa miradi mbalimbali ili wajue namna wanavyoweza kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza na kukuza biashara zao,” amesema Kuyukwa.
Ameeleza kuwa TIB inashirikiana kwa karibu na Serikali katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo ya taifa, hususan katika kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati kupata mitaji nafuu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na ajira.
Kuyukwa amesema lengo la benki hiyo ni kukuza miradi yenye tija na athari chanya kwa jamii ili wajasiriamali waweze kuimarika kiuchumi na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Ameongeza kuwa baada ya wajasiriamali kukua na kuimarisha biashara zao, wataweza kupata mikopo si tu kutoka TIB bali pia katika taasisi nyingine za kifedha, jambo litakaloongeza ushindani, kuimarisha sekta binafsi na kuchochea maendeleo endelevu nchini.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo, akiwemo mkulima wa mihogo katika Wilaya ya Handeni, Ramadhan Abdalah amesema baada ya kutembelea banda hilo anamatumaini ya kupata mtaji kwa ajili ya kilo cha biashara, wazo ambalo alikuwa nalo kwa muda mrefu lakini ameshimdwa kutekeleza kwa kuwa hakuwa na mtaji.
Mchimbaji mdogo wa madini Kalalani katika Wilaya ya Korogwe, Shabani Alex amesema kilio chao kikubwa ni mitaji na kwa kutembelea benki hiyo, huenda wakafikia ndoto zao za kufanya biashara hiyo kwa faida kubwa.
Mvuvi katika bahari ya Hindi Tanga, Mbwana Hassan amesema vifaa vya uvuvi vya kisasa ndio hitaji la wavuvi wengi na amefurahi kusikia benki hiyo inashughulika na uchumi wa buluu unaowalenga moja kwa moja wavuvi.