Msajili wa Baraza la Ushindani (FCT), Mhe. Mbegu Kaskasi,akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa wadau na wafanyabiashara mkoani Arusha ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya mfumo wa usajili wa mashauri kwa njia ya kielektroniki (e-filing).
ARUSHA:
Baraza la Ushindani (FCT) limewahimiza wadau na wafanyabiashara mkoani Arusha kutumia kikamilifu mfumo wa usajili wa mashauri kwa njia ya kielektroniki (e-filing), lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na kupunguza gharama katika uwasilishaji wa mashauri.
Akizungumza katika mafunzo hayo Msajili wa Baraza hilo, Mhe. Mbegu Kaskasi, alisema mfumo huo wa kisasa umeundwa ili kurahisisha usajili wa mashauri na rufaa bila wadau kulazimika kufika katika ofisi za FCT, hatua ambayo itaokoa muda na kuongeza ufanisi.
“Mfumo huu utaimarisha uwazi, kasi ya utoaji haki na kupunguza usumbufu kwa wadau,” alisema Mhe. Kaskasi, akibainisha kuwa hatua hiyo inakwenda sambamba na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma.”amesema Mhe.Kaskasi
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Moses Pesha, amelipongeza Baraza kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanaohusika na wananchi kwa ujumla, akisema hatua hiyo imeongeza uelewa na kuimarisha imani ya wananchi katika mifumo ya utoaji haki.
Naye Afisa TEHAMA wa FCT, Ndg. Athumani Kanyegezi, amesema mfumo wa e-filing unaimarisha usalama wa taarifa na kuongeza urahisi wa kuzifikia ndani ya muda mfupi, tofauti na mfumo wa zamani wa kuhifadhi mafaili kwa mikono.
Katika upande wa wadau, mfanyabiashara wa jijini Arusha, Bi. Jonia Karumuna, ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kuwezesha taasisi kama Baraza la Ushindani kuendelea kulinda haki za wafanyabiashara na kusikiliza rufaa zinazotokana na migogoro kutoka Tume ya Ushindani (FCC) na mamlaka mbalimbali za udhibiti ikiwemo EWURA, LATRA, TCRA, TCAA na PURA.
Amesema uwepo wa Baraza hilo umeongeza imani kwa wafanyabiashara kutokana na mchango wake katika kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya ushindani wa haki nchini.