WAZIRI WA VIWANDA JUDITH KAPINGA ARIDHISHWA NA VIWANGO VYA UZALISHAJI ALAF

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga amefanya ziara katika kiwanda cha ALAF Limited, kinachoongoza katika suluhisho mbalimbali za ujenzi Tanzania na kusema ameridhishwa na viwango vya uzalishaji kiwandani hapo.

Kapinga aliyekuwa ameongozana na viongozi wengine kutoka idara mbalimbali za wizara hiyo, alisema ALAF ni miongini mwa viwanda vya kuigwa kwani kimeonesha mfano halisi wa Tanzania yenye viwanda.

“Ubora wa bidhaa niliouona leo unathibitisha kuwa tunaweza kwani bidhaa hizi zinaweza kuuzwa hata nje ya nchi na kukidhi viwango vinavyotakiwa,” alisema na kuongeza kuwa serikali itaendelea kulinda viwanda vya ndani ili vizalishe kwa faida. 

Amefafanua uamuzi wa ALAF kuwekeza katika mtambo wa kuzalisha mabati ya rangi ambayo uzalishaji wake ulianza mwaka jana, ulikuwa sahihi kwani sasa watanzania wanaweza kuipata bidhaa hiyo kwa urahisi.

“Hapo awali nafahamu kuwa tulikuwa tunaagiza mabati haya kutoka nje ya nchi lakini sasa tunapata hapa hapa ALAF kwa urahisi na kwa haraka,” amesema na kuongeza kuwa uwepo wa mtambo huu umeongeza ajira kwa watanzania.

Amesema  serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika sekta hii ili kuhakikisha uzalishaji haukwami kwa namna yoyote kwa kushugulikia changamoto mbalimbali zinazoibuka kwa haraka ili pamoja na mambo mengine kuvutia uwekezaji zaidi.

“Milango yetu ikoa wazi kabisa na tunawahimiza mje tujadiliane pale ambapo mnapata changamoto ili tuzishugulikie kwa haraka kwa pamoja,” amesisitiza.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited Bibhu Nanda amemshukuru Waziri Kapinga kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuwa ALAF itaendelea kushirikiana na serikali kwa karibu ili malengo ya pande zote mbili yafikiwe kikamilifu.

“Lengo letu kuu ni kuendelea kuwa namba moja katika uzalishaji wa mabati na bidhaa nyingine za ujenzi kwani ndio kampuni kongwe ya mabati ambayo mwaka huu inaadhimisha miaka 63 tangu kuanzishwa kwake,” amesema.

Ametoa mwito kwa watanzania wajivunie bidhaa zinazozalishwa ndani hususani na kampuni ya ALAF.

ALAF Limited ni kampuni inayoongoza nchini Tanzania kwa kutengeneza mabati ya kuezekea nyumba. Ni kampuni iliyoanzishwa mwaka 1960, na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

ALAF imeunganisha kikamilifu operesheni, si tu kwa kutengeneza mabati, lakini pia kwa kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za uezekaji wa nyumba. ALAF Limited hutengeneza vifaa mbalimbali vya metali kwa matumizi mbalimbali ya uezekaji wa nyumba.

 Mwisho