Moloko kuibukia Ligi ya Championship

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mkongomani Jesus Ducapel Moloko amekamilisha usajili wa kujiunga na Mbeya Kwanza ya Tabora inayoshiriki Ligi ya Championship, baada ya kusaini mkataba hadi mwisho wa msimu huu.

Nyota huyo aliyewahi kuitumikia Yanga kuanzia Agosti 13, 2021 hadi Januari 28, 2024 akitokea AS Vita ya kwao DR Congo, amejiunga na Mbeya Kwanza baada ya kuachana na AS Kigali ya Rwanda.

Moloko alijiunga na AS Kigali Agosti 28, 2025 baada ya kuachana na ES Mostaganem ya Algeria, ingawa hakudumu nayo akiondoka Januari 2026, huku aliwahi kuchezea Diyala SC ya Iraq na Al Sadaqa Shahat SC ya Libya.

Nyota huyo anajiunga na kikosi hicho ambacho msimu huu kinanolewa na Maka Mwalwisi akienda kuongeza nguvu kwa kushirikiana na wachezaji wengine akisajiliwa kutokana na uzoefu wake.

Mbeya Kwanza iko nafasi ya tatu msimu huu katika Ligi ya Championship na pointi 34, nyuma ya Kagera Sugar iliyo ya pili na pointi 36, huku Geita Gold ikiongoza na pointi 37, baada ya timu zote kumaliza raundi ya kwanza kwa kucheza mechi 15.

Timu hiyo iliyouzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu uliopita, ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu kwenda Championship msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani baada ya kikosi hicho kukusanya pointi 25 tu.

Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, ikiwa na kazi ya kupigania nafasi ya kurejea tena Ligi Kuu Bara.