Singida Black Stars imekamilisha usajili wa aliyekuwa El Mahalla ya Misri, Raheem Shomary kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo huku mwenyewe akitaja sababu za kurudi Tanzania.
Rahim ambaye alitwaa tuzo ya mchezaji bora Chipukizi msimu wa 2023/24 akiwa na KMC amerudi Tanzania baada ya kucheza nusu msimu nchini Misri ambapo alisaini mkataba wa miaka mutatu.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa tayari wamekamilisha uhamisho wa beki huyo na muda wowote ataungana na timu tayari kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yao.
“Ni kweli mpango wa kuinasa saini ya beki huyo umekamilika baada ya makubaliano ya pande zote tatu tunatambua ubora na kipaji cha mchezaji huyo tunaamini tumefanya uamuzi sahihi kumrudisha ardhi ya Tanzania.”
Mwanaspoti lilimtafuta Shomari kuhusu taarifa hizo na akasema ni kweli, na anatarajia kurudi nchini kesho, Jumapili, tayari kwa ajili ya kuendelea na majukumu yake huku akidai kuwa fedha ndizo zimemtudisha Tanzania.
“Nacheza mpira kwa sababu ya fedha na zipo timu za Tanzania zinaweza kulipa vizuri kuliko timu za nje na zipo timu ambazo zina nafasi nzuri ya kumtangaza vizuri mchezaji kuliko nje,” amesema.
“Kuna wachezaji wamecheza Ligi ya Tanzania na wameenda kufanya vizuri Afcon hivyo naamini ata Ligi ya Tanzania ikishiriki kichuano ya kimataifa inatoa nafasi ya kumrangaza mchezaji nje sasa Singida Black Stars inafanya hivyo kimataifa naamini ni nafasi nzuri kwangu.”