Henry Mkanwa aanika mipango Gunners

KOCHA mpya wa Gunners FC ya jijini Dodoma, Henry Mkanwa amesema miongoni mwa malengo makubwa aliyopewa na uongozi wa timu hiyo ni kuhakikisha kikosi hicho kinabaki Ligi ya Championship msimu ujao, licha ya ushindani mkubwa uliopo.

Mkanwa aliyezifundisha Biashara United na Pamba Jiji, alipewa jukumu hilo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Juma Ikaba kusitishiwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili, kutokana na mwenendo mbaya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkanwa amesema anaijua vyema Ligi ya Championship kwa sababu sio mara ya kwanza kufundisha, ingawa, ili kufikia malengo ya kuendelea kukibakisha kikosi hicho msimu ujao anahitaji ushirikiano wa pamoja kikosini.

“Nafasi tuliyopo sio mbaya wala nzuri sana kwa sababu ya ushindani uliopo, naamini bado tuna uwezo wa kufanya vizuri kwa mechi za raundi ya pili, jambo kubwa ni kuhakikisha hatudondoshi pointi kizembe ili tufikie malengo,” amesema Mkanwa.

Ikaba aliyefundisha timu za Gwasa, Usalama na Baobab Queens, ameiongoza Gunners tangu ikiwa Ligi ya Mkoa (RCL) hadi Ligi ya Championship, ambapo inashika nafasi ya 12 na pointi 14, baada ya kushinda mechi tatu tu, sare tano na kupoteza saba.

Gunners imepanda Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kuongoza First League kundi B na pointi 35, baada ya kushinda mechi 11, sare miwili na kupoteza mmoja, ikiungana na kikosi cha Hausung kutoka Njombe iliyoongoza kundi A na pointi 25.

Baada ya timu hizo kuongoza makundi yao na kupanda Championship, zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa mpya wa First League kwa msimu wa 2024-2025 na kikosi hicho cha Gunners kilitwaa ubingwa huo kufuatia kuifunga Hausung mabao 3-0.