Serikali yashindwa kuwasilisha majibu shauri la Mwambe kunyang’anywa pasipoti

Dar es Salaam. Serikali imeshindwa kuwasilisha mahakamani majibu yake dhidi ya madai waziri wa zamani, Geofrey Mwambe katika shauri la kunyang’anywa hati za kusafiria, yeye na familia yake.

Badala yake imeomba iongezewe muda wa kuandaa na kuwasilisha majibu yake dhidi ya madai hayo, kabla ya usikilizwaji wa shauri hilo.

Mwambe ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mbunge wa Masasi CCM, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara anadai kunyang’anywa hati zake za kusafiria yeye familia yake na kuzuiliwa kusafiri nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, Mwambe akiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu amefungua shauri hilo la maombi Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika shauri hilo Mwambe naomba mahakama hiyo imruhusu kufungua shauri la mapitio ya mahakama ili mahakama hiyo imwamuru Kamishana wa Uhamiaji kuachia na kukabidhi hati zao hizo.

Mwambe amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura akidai hati hizo zinashikiliwa na Kamishna wa Uhamiaji  kinyume cha sheria na bila msingi wowote wa kisheria.

Katika hati hiyo ya dharura, mawakili Mpoki na Mwasipu wanathibitisha udharura wa shauri hilo wakidai kuwa usikilizwaji wake ni wa dharura ya hali ya juu sana kwa sababu, kwanza mwombaji, Mwambe ni mgonjwa na anatakiwa kusafiri kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, wanadai kuwa hawezi kusafiri kwa kuwa hati zake za kusafiria pamoja na za mke wake ambaye atasafiri naye kwa ajili ya kumhudumia kwa karibu, zimekamatwa na mjibu maombi wa kwanza, Kamishna wa Uhamiaji.

Hivyo wanadai kuwa kama maombi hayo hayatasikilizwa kwa dharura, hali yake ya afya itaendelea kudorora na kusababisha madhara makubwa kwake.

Shauri hilo lilitajwa mara ya kwanza Jumanne, Juni 20,2026 ambapo Mahakama iliwapa wajibu maombi siku mbili kuwasilisha majibu yao dhidi ya madai hayo badala ya siku 14 ambazo waliomba na mahakama ikapanga shauri hilo lisikilizwe leo Ijumaa, Januari 23, Jaji David Ngunyale.

Hata hivyo, mahakama haikuweza kulisikiliza kutokana na wajibu maombi kushindwa kuwasilisha majibu yao dhidi ya madai ya Mwambe, badala yake wameomba waongezewe muda mpaka Jumatatu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Daniel Nyakiha ameieleza mahakama kuwa wameshindwa kuwasilisha majibu yao kama mahakama ilivyolekeza kwa kuwa baada ya kupitia kwa kina kiapo cha mwombaji kuna watu wawili waliotajwa humo ambao mmoja yuko Sirari mkoani Mara na mwingine yuko Namanga, Arusha.

Amesema watu hao ni wahusika wakuu katika shauri hilo na kwamba ‎jitihada za kuwapata ndani ya siku mbili walizopewa ili kupata maelezo yao zimeshindikana.

“Hivyo tumeshindwa kupata majibu yanayoweza kuisaidia mahakama na tunaomba siku nne tuweze kuyawasilisha majibu yetu Jumatatu baada ya kupata hizo tarifa zao si tu haki itendeke, bali kuisaidia mahakama kutenda hiyo haki,” amesema Wakili Nyakiha.

Hata hivyo, amesema kuwa afisa huyo wa Uhamiaji kutokea Sirari japo kwa leo mawasiliano naye yamekuwa magumu lakini wanamtarajia kufika Dar es Salaam leo.

Wakili Mpoki amepinga nyongeza ya siku nne walizoomba akisema ni nyingi kwa kuzingatia kuwa kabla ya kufungua shauri hilo kwanza walimpelekea taarifa ya madai (demand notice) mjibu maombi wa kwanza, Kamishna Mkuu Uhamiaji, Desemba 31, 2025.

Amesema kama wajibu maombi wangeichukulia kwa uzito wangewenza kuifanyia kazi tangu walipoipokea muda huo ungetosha kupata taarifa wanazotaka.

‎Hivyo, amependekeza waongezewe siku mbili wawasilishe majibu yao ili shauri hilo lisikilizwe Jumatatu. 

‎Wakili Nyakiha, ameshukuru kuwa upande wa mwombaji hawajapinga maombi yao kuongezewa muda na kwamba naye akaomba wawasilishe majibu yao Jumatatu kama na shauri lisikilizwe Jumanne.

Hata hivyo, Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameiongezea Serikali siku mbili, akiwataka wajibu maombi wawasilishe majibu yapo Jumatatu , Januari 26, 2026 asubuhi na shauri lisikilizwe siku hiyo saa nane mchana.

Hati ya maombi ya shauri hilo inaungwa mkono na kiapo cha Mwambe mwenyewe na kiapo cha mdogo wake, Nestory Chilumba, ambapo anasimulia namna alivyonyang’anywa hati zake za kusafiria na za familia yake wakiwa safarini kuelekea Nairobi nchini Kenya na kisha Ujerumani.

Kwa mujibu wa kiapo chake, Mwambe ambaye ni Mtanzania na mmiliki wa hati ya kusafiria namba TDE011349 na mkewe Tumaini Jason Kyando anamiliki hati ya kusafiria namba TAE181501.

Pia, kuna watoto wao watatu ambao bado ni wadogo, Kinkil Geoffrey Mwambe, anayemiliki hati ya kusafiria namba TAE923387; Karen-pracht Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE925212 na Kathrin-lena Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE903654.

Desemba 17, 2025, alikuwa anasafiri kuelekea Ujerumani kupitia Kenya kwa ajili ya matibabu.

Katika kituo cha mpaka cha Namanga, aliwasilisha hati zake za kusafiria kwa madhumuni ya kupata muhuri wa kutoka Tanzania ili apate muhuri wa kuingia Kenya na kuendelea na safari yake kwa matibabu.

Alichagua kutumia njia ya Kenya kwa kuwa taratibu za kupata Visa ya Schengen ni rahisi, za haraka na zenye ufanisi zaidi ikilinganishwa na taratibu zilizopo Dar es Salaam ambazo huchukua muda mrefu zaidi.

Pia, mke wake na watoto wao watatu walitarajiwa kusafiri kupitia kituo cha mpaka wa Sirari wilayani Musoma, kwa nia ya kwenda likizo za Krismasi katika Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara, na baadaye kuungana naye Nairobi kwa ajili ya maombi ya Visa ya Schengen.

Hivyo, siku hiyo alimkabidhi hati yake ofisa Uhamiaji mmoja aitwaye Patrick Mkande, na baada ya muda mfupi, ofisa huyo alimwambia kuwa hati yake inaonesha kuwa yeye ni mtumishi wa umma na hivyo anahitaji kibali cha mwajiri kusafiri nje ya nchi.

Mwambe alikataa kuwa kwa sasa si mtumishi wa umma tena (mbunge) na ofisa huyo alimuomba asubiri ili awasiliane na mkuu wake juu ya tofauti ya hadhi iliyoonekana kwenye hati yake kutoka kuwa mtumishi wa umma hadi raia wa kawaida, kwa kuwa watumishi wa umma huhitaji kibali cha kusafiri.

Iilichukua zaidi ya saa saba na ofisa huyo alimweleza kuwa mpaka muda huo hakuna jambo lolote lililokuwa limefanyika kuhusu uhakiki wa hati hiyo.

Hivyo, Mwambe alilazimika kurudi Dar es Salaam kwa kuwa kuendelea kubaki Namanga katika hali yake ya ugonjwa kulikuwa na madhara kwa afya yake.

Alipomuomba ofisa huyo amrudishie hati yake ili arudi Dar es Salaam na kupata ufafanuzi zaidi na maofisa wa uhamiaji, ofisa huyo alikataa.

Hali kama hiyo hiyo iliwakuta mkewe na watoto wao watatu waliokuwa wakivuka katika kituo cha mpaka cha Sirari, ambapo pasipoti zao zilikamatwa na maofisa wa uhamiaji, nao wakaamua kurudi Dar es Salaam.

Alipowasili Dar es Salaam akiwa mgonjwa, aliwaomba wakili wake Hekima Mwasipu na mdogo wake Nestory Chilumba waende kuchukua pasipoti hizo kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji katika ofisi yake ya Kurasini, Desemba 24, 2025.

Kamishna baada ya kuwasiliana na maofisa wa Uhamiaji katika vituo husika vya mipakani, walimweleza kuwa pasipoti hizo zilichukuliwa na maofisa hao katika vituo hivyo na akawaahidi kulifanyia kazi suala hilo kubaini sababu za kukamatwa na kuchukuliwa kwa hati hizo.

Hata hivyo mpaka anaapa kiapo hicho kufungua shauri hilo, Kamishna alikuwa hajamjibu wala kumpa sababu zozote za kukamatwa na kuchukuliwa kwa hati zao.

Anasisitiza kuwa kitendo cha kukamata na kuendelea kuhifadhi hati hizo za kusafiria kinyume cha sheria kimemnyima haki yake ya Kikatiba ya uhuru wa kusafiri.