Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kaloleni na Shule ya Sekondari ya Msasani zinazozunguka Mlima wa Kilimanjaro walioshiriki zoezi la kupanda miti na kupata mitungi ya gesi , kutoka kampuni ya Taifa gas kwenye programu ya utunzaji wa mazingira ya ‘Guardians of the Peak 2026’

Meneja Masoko wa Kampuni ya Taifa gas , Oscar Shelukindo akigawa mtungi wa gesi kwa mmoja wa washiriki wa programu ya uhifadhi wa mazingira ‘Guardians of the Peak 2026’ iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro

Wanafunzi wa sekondari ya Msasani ya Manispaa ya Moshi wakiwa kwenye zoezi la upandaji wa miti na kujifunza utunzaji wa mazingira katika programu ya ‘Guardians of the Peak 2026’ iliyodhaminiwa na kampuni ya Taifa gas

Meneja Masoko wa Kampuni ya Taifa gas wa tatu kushoto , Oscar Shelukindo baada ya zoezi la kupanda miti na kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali kwenye programu ya ‘Guardian of the Peak 2026’ iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro

Wanafunzi na wadau mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya zoezi la upandaji wa miti na kujifunza kuhusu nishati safi ya kupikia kwenye kilele cha programu ya ‘Guardians of the Peak 2026’ iliyofanyika Mkoani Kilimanjaro

Meneja Masoko wa Taifa Gas , Oscar Shelukindo akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti na uhifadhi ya mazingira katika programu’ Guardians of the Peak 2026’ Mkoani Kilimanjaro.
**
Kampuni ya usambazaji wa gesi nchini, Taifa Gas imedhamini programu ya kutangaza vivutio vya utalii nchini duniani na uhifadhi wa mazingira kupitia kupanda mlima Kilimanjaro ijulikanayo kama Guardians of the Peak msimu wa pili itakayofanyika kuanzia Januari 20-31, 2026 yenye kauli mbiu “Embrace Clean Energy, Protect Tomorrow”.
Kupitia programu hii mbali na washiriki kupanda Mlima Kilimanjaro pia watashiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti, kupatiwa elimu juu ya mabadiliko ya tabia nchi na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya ukataji kuni na mkaa.
Akiongelea udhamini wa programu hii, Meneja wa Taifa Gas, Davis Deogratius amesema udhamini huu ni mwendelezo wa kampuni ya Taifa Gas kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepukana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira kwa ajili ya kulinda mazingira na afya za wananchi.
“Kupitia programu hii,Taifa Gas tumedhamini wanafunzi na baadhi ya wafanyakazi wetu kushiriki kupanda mlima Kilimanjaro vilevile kushiriki zoezi la kupanda miti katika sehemu mbalimbali za halmashauri ya mji wa Moshi,kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali na kuwagawia mitungi ya gesi”, amesema Deogratius.
Amesema Taifa Gas imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Serikali kulinda mazingira kupitia uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na usambazaji wa gesi katika makundi mbalimbali ya jamii katika sehemu za mijini na vijijini nchini kote na imekuwa ikitunukiwa tuzo mbalimbali za heshima za utunzaji mazingira kutoka Serikali na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Taifa Gas imedhamini programu hii ya vijana ya Guardians of the Peak katika hatua za kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.
Guardians of the Peak msimu wa pili inajumuisha wadau mbalimbali wa mazingira na utalii na wataalamu wa kuandaa makala za utalii (Documentary) zitakazotumika kutangaza vivutio vya utalii katika soko la China na duniani kote sambamba na uhamasishaji wa utunzaji wa mlima Kilimanjaro na kuhamasisha utali wa ndani.