YANGA imeruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili ikikubali kuchapwa 2-0 na Al Ahly katika mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, leo Ijumaa, lakini makosa mawili tu ya wachezaji binafsi ndiyo yaliyowagharimu.
Hicho ni kipigo cha kwanza kwa Yanga katika kipindi cha miezi minne tangu Oktoba 18, 2025.
Yanga iliruhusu bao la kwanza kwenye kipindi cha kwanza baada ya beki wa kulia, Israel Mwenda kushindwa kumkaba Trezeguet, aliyefunga kwa kichwa, kabla ya kuruhusu bao la pili kipindi cha pili na kiungo Duke Abuya alipoteza mpira na Al Ahly kutumia nafasi hiyo kwa sababu Yanga ilikuwa haina kwenye muundo mzuri na hivyo, Trezeguet akawaadhibu tena kwa shuti la kuzungusha.
Kipute hicho kilipigwa kwenye Uwanja wa Al Salam, Cairo, Misri.
Tofauti na ilivyokuwa katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alifanya mabadiliko ya kikosi cha kwanza katika maeneo mawili tofauti, Djigui Diarra (Abuutwalib Mshery) alirejea langoni pamoja na Mwenda (Kibwana Shomary) upande wa beki ya kulia.
Eneo lingine ni upande wa ushambuliaji ambao alianza na Laurindo Dilson ‘Depu’ ambaye alifunga na kutoa asisti dhidi ya Mashujaa badala ya Prince Dube huku Pacome Zouzoua naye akianzia benchi.
Pedro aliamua kuanza na mabeki watatu wa kati hivyo Yanga ilibadilika kimuundo kutoka 4-2-3-1 hadi 3-5-2, mpango ambao ulionekana kufanya kazi vizuri dakika 45 za kipindi cha kwanza licha ya kuruhusu bao katika dakika za nyongeza kabla ya mapumziko (45+3) ambalo lilifungwa kwa kichwa na Trezeguet kutokana na krosi ya Mohamed Hany.
Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Yanga ilionekana kuwa bora katika kujilinda na kushambulia huku ikipiga mashuti manne sawa na wenyeji wao kati ya hayo mawili yalilenga lango tofauti na Ahly ambao ni shuti moja tu ambalo lililenga lango.
Yanga ilirejea kipindi cha pili na kufanya mabadiliko mawili kwa mpigo, walitolewa Mwenda na Damaro ambaye tayari alikuwa na kadi ya njano huku wakiingia Pacome na Mudathir Yahya.
Mabadiliko ambayo Yanga ilifanya kipindi cha pili hayakuonekana kuwa na afya, zaidi timu ilionekana kuwa wazi nyuma wakati wakitafuta bao la kusawazisha, kiasi cha kuruhusu nafasi tatu za hatari huku moja ikizaa bao la pili na ushindi wa wenyeji.
Uwepo wa Pacome na kuongezwa kwa Dube katika safu ya ushambuliaji kulipunguza nguvu ya timu katika kujilinda.
Kwa kutambua hilo ndio maana Pedro aliamua kufanya mabadiliko ya lazima kwa kuwatoa Boka na Job huku wakiingia Mohammed Hussein na Yao.
Licha ya nyota hao kuongeza utulivu tayari Yanga ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 na hata juhudi za kusawazisha zilishindwa kuzaa matunda.
Mara ya kwanza Yanga kucheza ugenini dhidi ya Al Ahly ilikuwa Machi 15, 2009 na ilikumbana na kipigo kizito cha mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa Cairo.
Machi 9, 2014, Yanga ilirejea tena Cairo ikiwa na matumaini baada ya kushinda bao 1-0 nyumbani kupitia Nadir Haroub ‘Canavaro’, lakini matumaini hayo yalififia baada ya Al Ahly kushinda bao 1-0 katika dakika 90 za mchezo wa marudiano.
Hatimaye, Waarabu hao waliibuka na ushindi wa penalti 4-3 na kuiondosha Yanga katika michuano hiyo.
Katika msimu wa 2016, Yanga ilicheza tena ugenini dhidi ya Al Ahly Aprili 20 na ilipoteza kwa mabao 2-1.
Hata hivyo, tofauti na michezo ya awali, Yanga ilionyesha upinzani mkubwa zaidi, ikifunga bao ugenini, japokuwa haikutosha kuzuia kipigo kingine ugenini.
Baada ya miaka minane kupita, 2024, Yanga ilikutana tena na Al Ahly huko Misri katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, wakiwa kundi D, Yanga ilipoteza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Hussein El Shahat hata hivyo ilimaliza hatua hiyo ikiwa na pointi nane ikishika nafasi ya pili nyuma ya vigogo hao na kuweka rekodi kwa kutinga robo fainali.
Kwa jumla, katika michezo hiyo ya ugenini dhidi ya Al Ahly, Yanga imeruhusu mabao tisa, ikifunga bao moja pekee, takwimu zinazoonyesha ugumu wa kuvunja ngome ya Waarabu hao wanapocheza nyumbani kwao.
Rekodi hiyo ya ugenini imeifanya mechi yoyote kati ya timu hizo Misri kuwa mtihani mkubwa kwa Yanga, hasa ikizingatiwa Al Ahly mara nyingi hutumia vyema faida ya uwanja wao pamoja na uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa.
Baada ya matokeo hayo, Yanga sasa inarejea nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya kukabiliana tena na wababe hao wikiendi ijayo, Januari 30 huko visiwani Zanzibar huku wakiwa na matumaini ya kulipa kisasi kwenye Uwanja wa Amaan.
Vikosi vilivyoanza, Al Ahly; Shobeir, Ashour, Atef, Attia, Dieng, Hany, Ibrahim, Kouka, Otaka, Trezeguet na Zizo.
Yanga; Diarra, Mwenda, Boka, Hamad, Job, Mwamnyeto, Damaro, Abuya, Depu, Nzengeli na Okello.