NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Deniss Londo, amesema kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO),vijana wabunifu wanapata fursa ya kubadili mawazo yao ya kiteknolojia na ujasiriamali kuwa bidhaa na huduma zenye tija katika soko.
Amesema viwanda vina mchango mkubwa katika utoaji wa ajira, kuimarisha usalama wa kiuchumi na kukuza ubunifu, hususan kwa vijana.
Ameyasema hayo leo Januari 23, 2026 Jijini Dar es Salaam alipotembelea ofisi za TIRDO ambapo amefurahishwa na shughuli inayofanywa na shirika hilo hasa utafiti kwenye maendeleo ya viwanda nchini.
Amesema kuwa jukumu la TIRDO si kuanzisha viwanda moja kwa moja, bali ni kufanya utafiti, kusambaza teknolojia na kusaidia wazalishaji wadogo na wa kati kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija.
Aidha amewapongeza viongozi na wataalamu wa TIRDO kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulea wajasiriamali waliotoka ngazi ya chini hadi kufikia uzalishaji wa viwandani ambapo kuvutiwa na miradi ya urejelezaji wa taka za plastiki pamoja na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, akisema miradi hiyo inalinda mazingira na wakati huo huo kuleta ajira kwa wananchi.
Hata hivyo amesema kuwa ushirikiano kati ya wizara, taasisi za umma na mamlaka za serikali za mitaa ni muhimu ili kuhakikisha miradi ya viwanda inatekelezwa kwa kuzingatia sera, viwango na mahitaji halisi ya wananchi. Ameahidi kuyafikisha mapendekezo ya wadau katika ngazi ya wizara kwa lengo la kuyaendeleza katika maeneo mbalimbali nchini.
Pamoja na hayo amesema kuwa maendeleo ya viwanda bado ni nguzo kuu ya ukombozi wa kiuchumi wa Tanzania, akisisitiza kuwa bila uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya viwanda, taifa haliwezi kufikia maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Mtambo, amesema kuwa wanatarajia kuanzisha kituo cha kutengeneza na kufanyia matengenezo vifaa vya kielektroniki kwa ajili ya kukuza ubunifu wa ndani na kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje.


















