Unguja. Zanzibar imepiga hatua muhimu kuelekea uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baada ya kusaini mkataba wa ukusanyaji wa takwimu za mtetemo kwa teknolojia ya kisasa ya 3D seismic survey.
Mkataba huo wa takribani mwaka mmoja umesainiwa kati ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) na Kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS), yenye makao yake makuu nchini Oman.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mkataba huo leo Januari 24, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa ZPDC, Mikidadi Ali Rashid, amesema hatua hiyo ni ya kihistoria na inaweka msingi madhubuti wa mwelekeo wa baadaye wa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia visiwani Zanzibar.
Amesema ukusanyaji wa takwimu za mtetemo kwa njia ya 3D utasaidia kupata taarifa sahihi za kijiolojia zitakazowezesha kufanya maamuzi yenye tija kuhusu uwekezaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.
“Utafiti huu utaipatia Zanzibar ramani ya kina ya miamba iliyo chini ya ardhi na hivyo kuongeza uwezekano wa kugundua maeneo yenye akiba ya mafuta na gesi kwa uhakika zaidi,” amesema Rashid.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC), Mikidadi Ali Rashid (kulia) na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS) yenye makao makuu yake nchini Oman, wakisaini nyaraka za mkataba wa ukusanyaji wa taarifa za mtetemo za mafuta na gesi asilia za 3D Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Kwa mujibu wa ZPDC, utekelezaji wa mkataba huo unatarajiwa kuongeza imani ya wawekezaji, kukuza sekta ya nishati na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar kupitia ajira, mapato ya serikali na uboreshaji wa miundombinu.
Hatua hiyo inaifanya Zanzibar kujiunga na maeneo mengine barani Afrika yanayotumia teknolojia ya kisasa katika utafiti wa rasilimali za mafuta na gesi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha usalama wa nishati na maendeleo endelevu.
Akizungumza baada ya hafla ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri Masoud amesema ushirikiano kati ya Kampuni ya Africa Geophysical Services (AGS) na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) unalenga upatikanaji wa takwimu muhimu zitakazoiwezesha Zanzibar kufikia hatua inayofuata ya utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
“Tukio la leo la kusaini mkataba kati ya AGS na ZPDC limejikita katika kupata data zitakazotuwezesha kwenda kwenye hatua nyingine muhimu ya uchimbaji wa mafuta na gesi, au gesi pekee au mafuta pekee. Hatua hii ni muhimu sana kwa mustakabali wa sekta hii,” amesema Waziri Masoud.
Amezipongeza taasisi za ZPDC na AGS kwa kufanikisha ushirikiano huo, akisema haikuwa safari rahisi hadi kufikia hatua ya kusaini mkataba huo, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya pande zote katika kuendeleza sekta ya nishati.
Waziri Masoud amesema utekelezaji wa kazi hiyo utafanyika katika mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja, na amewaomba wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa taasisi zitakazohusika ili kuhakikisha shughuli hiyo inatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya maendeleo ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa, pamoja na mafuta na gesi, sekta ya Uchumi wa Buluu inahusisha pia rasilimali za baharini, akibainisha kuwa Serikali ina mipango mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ili iwe chachu ya maendeleo ya kiuchumi.
“Hivyo, tunaiomba AGS kushirikiana kwa karibu na ZPDC na Serikali kwa ujumla ili kazi hii iweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa kwa maslahi mapana ya nchi,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa AGS Tanzania, Shaun Graham, amesema kampuni hiyo imefurahishwa kupata fursa ya kushiriki katika mradi huo muhimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika utafutaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia.
Amesema mkataba huo utaipa ZPDC uwezo wa kupata taarifa za kina zitakazosaidia katika matumizi na usimamizi wa rasilimali hizo kwa manufaa ya taifa.
Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZPDC kwa kuwaamini na kuwapa dhamana ya kushirikiana katika kazi hiyo ya utafiti wa mafuta na gesi asilia, akiahidi kuwa AGSxxxxx itatekeleza majukumu yake kwa viwango vya juu vya kitaalamu.