Simba katika hesabu za kupindua msimamo CAF

HESABU za mzunguko wa kwanza katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Esperance na Simba zinafungwa leo Jumamosi zitakapokutana kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi, jijini Tunis.

Ni mechi ya mtego kwa timu zote, huku ikiwa ngumu zaidi kwa Simba inayoburuza mkia bila ya pointi wakati mpinzani wake inazo mbili. Kuanzia saa 1:00 usiku kwa majira ya Afrika Mashariki, kipute hicho kitaanza, kikichezeshwa na mwamuzi Jean-Pierre Nguiene Bissila kutoka DR Congo. Dua za Wanasimba na Watanzania kwa jumla zinahitajika kwa Simba kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Simba inashuka dimbani leo baada ya jana Ijumaa wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Yanga walikuwa Misri kukabiliana na Al Ahly ikiwa ni mechi ya kundi B.

Kesho Jumapili, kuna wawakilishi wetu wengine wawili wanaoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika wakijitupa uwanjani. Azam ipo Kenya kucheza dhidi ya Nairobi United kuanzia saa 10 jioni, huku Singida Black Stars ikiikaribisha AS Otoho ya Congo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

TUNI 04


Vuta pumzi kwanza. Wikiendi hii si mitanange hiyo tu pekee, bali kuna mechi kibao za kusisimua zinazotolewa macho na wapenda kabumbu duniani kupitia michuano mbalimbali.

Ukiweka kando michuano hiyo ya CAF ngazi ya klabu iliyorejea baada ya kupisha Fainali za AFCON 2025, Ulaya wikiendi hii kinawaka pale England ikisubiriwa mechi kali kati ya Arsenal dhidi ya Manchester United itakayopigwa kesho Jumapili.

Lakini leo Jumamosi, bingwa mtetezi wa Premier, Liverpool itahitimisha siku kwa kucheza ugenini dhidi ya Bournemouth majira ya saa 2:30 usiku kwani kabla ya hapo, saa 9:30 alasiri itapigwa mechi ya kwanza West Ham ikicheza dhidi ya Sunderland, kisha saa 12:00 jioni kuna mechi tatu ikiwamo ya Manchester City dhidi ya Wolves.

Leo pia Villarreal itaikaribisha Real Madrid katika La Liga na ligi hiyo zitapigwa mechi nne Jumamosi hii.

Bundesliga, Serie A na hata Ligue 1, leo Jumamosi kinawaka vibaya mno huko. Unachotakiwa ni kutuliza macho, kuangalia wapi panakupendeza, ule burudani.

TUNI 02


Pointi mbili za Waarabu hao wa Tunisia zilizotokana na sare mechi za awali dhidi ya Stade Malien (0-0) nyumbani na Petro Atletico (1-1) ugenini, zinawaumiza vichwa wanapokwenda kukabiliana na Simba iliyojeruhiwa nje na ndani.

Simba ilianza kufungwa 1-0 nyumbani na Petro Atletico, kisha ikaenda kufungwa 2-1 na Stade Malien nchini Mali.

Hesabu za Wanamsimbazi sasa ni kupata pointi leo dhidi ya Esperance ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali ya michuano ya CAF kwa mara ya nane katika misimu tisa tangu 2018.

Rekodi nzuri ya Simba kufuzu robo fainali michuano ya CAF mara saba katika kipindi cha kuanzia 2018 kila inapoingia makundi, inaweza kuwafanya nyota wa kikosi hicho kuingia na tumaini jipya, lakini haitakuwa rahisi kwao kutokana na aina ya mpinzani inayekwenda kukabiliana naye.

Esperance yenye mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyobeba 1994, 2011, 2018 na 2019, inapambana kurudisha makali yake huku ikiwa na kumbukumbu ya kukosa ubingwa mwaka 2024 ilipopoteza fainali mbele ya Al Ahly, kabla ya msimu uliopita 2025 kuishia robo fainali.

Tangu mara ya mwisho ibebe taji la michuano hiyo, Esperance haijawahi kuishia makundi, ilikwamia robo fainali 2020, nusu fainali (2021), robo fainali (2022), nusu fainali (2023), nafasi ya pili (2024) na robo fainali (2025).

TUNI 03


Simba iliyocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kupoteza mbele ya RS Berkane, kuanza kwao vibaya msimu huu hatua ya makundi si jambo geni, imewahi kufanya hivyo msimu wa 2022–2023 katika Ligi ya Mabingwa ikipoteza mechi mbili za kwanza, lakini ikatoboa.

Msimu huo ikiwa kundi C, ilianza kufungwa bao 1-0 na Horoya ugenini, kisha ikapokea kichapo cha 3–0 nyumbani dhidi ya Raja Athletic. Baada ya hapo, Simba ikashinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Vipers (1-0) ugenini na nyumbani, kisha ikaichapa Horoya 7-0 nyumbani. Ikaenda Morocco kuhitimisha ratiba kwa kufungwa 3-1 na Raja Athletic, ikafuzu kwa pointi tisa ikiizidi Horoya iliyokuwa na saba na Vipers (2), wakati Raja ikiwa kinara na 16.

Ikitokea Simba imepoteza leo, maana yake ni itatakiwa kushinda mechi zote tatu za duru la pili hatua ya makundi ili kufikisha pointi tisa, huku ikiomba wapinzani wake wawili kati ya watatu, wasivuke pointi nane.

Kwa sasa Simba ikiwa inaburuza bila pointi, Petro Atletico na Stade Malien zipo juu pale kila moja ina pointi nne, huku Esperance inazo mbili.

Mechi ya Stade Maline na Petro Atletico hapo kesho pengine itatoa majibu ya haya yote ikitokea Simba itapoteza leo.

Lakini kama Simba itapata pointi yoyote leo iwe kushinda au sare, maana yake itakuwa bado katika matumaini makubwa ya kufuzu robo fainali japo itatakiwa kushinda mechi tatu zijazo ikianza na Esperance nyumbani, kisha Petro Atletico ugenini na kumalizia nyumbani dhidi ya Stade Malien.

TUNI 01


Ukiachana na Simba kutokuwa na matokeo mazuri kwa siku za karibuni hali iliyofanya kutokuwa na utulivu ndani ya klabu hiyo, lakini kuna matumaini yameibuka baada ya usajili uliofanyika.

Kurejea kwa Clatous Chama aliyekuwa chachu ya Simba kufanya vizuri hasa msimu wa 2018-2019 mara ya kwanza kiungo huyo kutua hapo na kuivusha robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, kimewashusha pumzi Wanamsimbazi.

Licha ya kwamba Chama hataweza kuwa kama yule wa miaka nane iliyopita alipoanza kuichezea Simba, lakini ubora wake katika kutengeneza nafasi na kufunga haujapungua. Amefanya hivyo akiwa Yanga na Singida Black Stars, timu alizozitumikia baada ya kuondoka Simba 2024.

Mbali na Chama, Simba pia imeimarisha ukuta wake kwa kusajili kipa Djibrilla Kassali aliyechukua nafasi ya Moussa Camara ambaye ni majeruhi. Imesajili mabeki wawili, Nickson Kibabage upande wa kushoto na Ismael Olivier Toure anayecheza kati. Pia kuna winga Libasse Gueye, huku wakiondoka Jean Charles Ahoua na Steven Mukwala, Chamou Karaboue waliokuwa kikosi cha kwanza.