Waarabu wengine wapiga hodi Simba wakitaka winga

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mzambia Joshua Mutale yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na Al Adalah Club ya Saudi Arabia, baada ya mabwenyenye hao wanaoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kuonyesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo kwa mkopo.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 1, 2024, akitokea Power Dynamos ya kwao Zambia, ni miongoni mwa wachezaji ambao watatolewa kwa mkopo dirisha hili dogo, ili kutoa pia nafasi kwa wengine kuingia kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Mwanaspoti linatambua nyota huyo hayupo katika mipango ya kocha mkuu wa timu hiyo, Steve Barker na awali ilidaiwa huenda angejiunga kwa mkopo Kenya Police FC ya Kenya, ili akaungane na mchezaji mwenzake, Awesu Awesu aliyetimkia huko.

MUTA 01


Hata hivyo, baada ya dili la nyota huyo kwenda Kenya kuonekana gumu, Al Adalah Club iliyoanzishwa mwaka 1984, ikiwa na miaka 42, imeonyesha nia ya kumhitaji ili kuitumikia kwa mkopo, huku kukiwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja.

MUTA 03


Katika Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia msimu huu, Al Adalah Club inashika nafasi ya 15 na pointi 14, kati ya timu 18 zinazoshiriki, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tatu tu, sare mitano na kupoteza tisa, ikifunga mabao 21 na kuruhusu 33.

MUTA 02


Mutale ni miongoni mwa nyota wanaokatwa katika kikosi hicho kwa ajili ya kupisha nafasi ya wachezaji wengine wa kigeni wanaoendelea kusajiliwa kwenye dirisha hili dogo, lililofunguliwa Januari 1, 2026 hadi litakapofungwa Januari 30, 2026.