Matokeo Simba SC yamuibua mkongwe

MATOKEO yasiyoridhisha inayoendelea kuyapata Simba kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, yamemuibua nyota wa zamani wa timu hiyo, Amir Maftah ambaye ameungana na mashabiki kutoa mtazamo wake.

Simba imepoteza alama tano katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu baada ya kufungwa 2-0 na Azam FC na sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar wikendi iliyopita. Pia imepoteza michezo yote miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Real Bamako ya Mali.

Mwenendo huo wa klabu hiyo umezua maswali na kuleta wasiwasi kwa baadhi ya wanachama, mashabiki na baadhi ya wachezaji wa zamani ambao wamekuwa wakipaza sauti kwa uongozi kufanya jambo ili kuokoa hali hiyo.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Amir Maftah aliliambia Mwanaspoti kuwa kinachoendelea klabuni hapo hakiwafurahishi mashabiki na kinapaswa kuwa funzo kwa viongozi ambao wanapaswa kujitathmini na kutafuta haraka mwarobaini wa tatizo hilo ili kuirejesha katika njia nzuri.


“Hiki ni kipindi ambacho uongozi, wachezaji na mashabiki wanatakiwa wawe kitu kimoja ili kujenga timu yao irudi katika hali nzuri zaidi,” alisema Maftah.

Alishauri uongozi wa klabu hiyo kutumia vyema dirisha dogo la usajili litakalofungwa Januari 30, mwaka huu, kwa kusajili wachezaji wa maana wenye uzoefu ambao wataongeza kitu kwenye timu yao kuliko kung’ang’ania wachezaji ambao hawana msaada kwa timu.

“Wanatakiwa wafanye usajili kwa sababu kuna wachezaji wametoka ambao walikuwa muhimu akiwemo Tshabalala (Mohamed Hussein). Waangalie wachezaji waliokomaa kwasababu hiii ni timu kubwa na ili iwe bora kama zamani ni lazima waangalie aina ya wachezaji walionao,” alisema mkongwe huyo.

Naye, Katibu wa Simba tawi la Mkuyuni jijini Mwanza, Hashim Kasisiko alisema viongozi ndiyo chanzo cha matatizo yanayoikumba timu hiyo kwa sasa kutokana na kushindwa kufanya usajili unaoeleweka ambao kila msimu unawalazimu kujenga upya timu yao.

“Simba ili irudi katika hali yake ya zamani wanatakiwa kuzingatia safu ya viongozi na wachezaji vinginevyo wataendelea kusajili wachezaji na kubadili makocha,” alisema Kasisiko.


Kwa upande wake, mwanachama wa timu hiyo, Sadru Salim alisema changamoto inazopitia klabu yao ni za mpito kama ilivyo kwa timu yoyote duniani, huku akisisitiza viongozi kujitambua ili kuzitafutia ufumbuzi.

Ameongeza kuwa hali hiyo pia inachochewa na mpasuko uliopo kati ya viongozi na wanachama kwani baadhi ya viongozi hawakubaliki na wanapaswa kuwajibika kwa kinachoendelea klabuni.

“Viongozi wanapaswa kutambua nini kinahitajika kwa wanachama na viongozi, hata hivyo, baadhi yao hawakubaliki hivyo wawape wanachama haki yao kwa kujizulu au kuitisha mkutano wa uchaguzi ili kuchagua viongozi wengine wenye maono mapya,” alishauri Salim.