Kutokana na historia yake ndefu, kuanzia jamii za kale za Paleo-Inuit, wavumbuzi wa Ulaya, hadi uwapo wa kijeshi wa Marekani katika Vita Baridi, Greenland imejenga msingi thabiti wa umuhimu kimkakati.
Hata hivyo, karne ya 21 imeibua sura mpya ya kisiwa hiki: Si tu kama alama ya ustahimilivu wa binadamu, bali kama kitovu cha nguvu, rasilimali na mvutano wa kimataifa.
Hapa, nafasi yake ya kijiografia, mabadiliko ya tabianchi na rasilimali za madini zinachangia moja kwa moja masilahi ya mataifa makubwa, hasa Marekani, kuzingatia kisiwa hiki kama kipengele kisichoweza kupuuzwa katika siasa na usalama wa dunia.
Sasa kisiwa cha Greenland, chenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba milioni 2.17, ambacho karibu asilimia 80 ya eneo lake limefunikwa na barafu, kinashikilia nafasi muhimu zaidi kuliko wakati wowote.
Kisiwa hiki kimekuwa kiini cha usalama wa Marekani, uwanja wa rasilimali za teknolojia za kisasa, na shina la mvutano wa kisiasa kati ya mataifa makubwa.
Katika karne hii, kushindwa kuielewa Greenland si tu ni kupuuza historia yake, bali pia ni kupuuza mustakabali wa siasa za kimataifa na usalama wa dunia kwa ujumla.
Katika karne ya 21, Greenland imeibuka kutoka kivuli cha historia yake ndefu na baridi kali na kuwa kitovu cha mjadala wa kimataifa kuhusu usalama, rasilimali, na haki ya kujitawala.
Greenland iko katikati ya Arctic, eneo la kaskazini la dunia, ikidhibiti njia muhimu kati ya Amerika Kaskazini na Ulaya.
Kwa mujibu wa ‘Encyclopaedia Britannica’, nafasi hii ya kijiografia inafanya Greenland kuwa kituo muhimu cha ulinzi wa Atlantiki ya Kaskazini na ufuatiliaji wa mapema wa makombora yanayoweza kulenga Mashariki ya Marekani.
Njia fupi zaidi za makombora ya masafa marefu kutoka Asia au Russia kuelekea Marekani hupitia juu ya Arctic, jambo linaloipa Greenland umuhimu wa kipekee wa kijeshi.
Kuwapo kwa Pituffik Space Base, kituo cha kijeshi cha Marekani huko Greenland, kunaakisi mantiki hii. Kituo hiki kinatumika katika mifumo ya tahadhari ya mapema na ufuatiliaji wa anga za juu, kikifanya Greenland kuwa sehemu hai ya usanifu wa ulinzi wa Marekani.
Tangu kumalizika kwa Vita Baridi, Marekani haikuondoka Greenland na badala yake, ilibadilisha mkazo wake kutoka tishio la nyuklia kwenda ufuatiliaji wa anga, satelaiti na usalama wa kimkakati wa Arctic.
Katika vitabu vya sera za ulinzi vya karne ya 21, Greenland hutajwa kama “eneo lisiloweza kuepukika” katika hesabu za usalama wa Marekani.
Kauli za kisiasa kutoka Washington ikiwamo mijadala ya umma kuhusu uwezekano wa Marekani kuipata Greenland hazipaswi kuchukuliwa kama matangazo ya kisheria, bali kama ishara ya uzito wa kimkakati wa kisiwa hicho. Kauli hizo zimezua mijadala kati ya Denmark, Umoja wa Ulaya (EU) na jumuiya ya kimataifa.
Ushindani wa Russia, China na Nato
Karibu tangu mwisho wa Vita Baridi, Arctic imegeuka kuwa uwanja mpya wa ushindani wa kimataifa. Russia imeongeza uwepo wake wa kijeshi katika maeneo ya kaskazini, ikijenga vituo vipya na kufufua miundombinu ya zamani.
China, kwa upande wake imetangaza hadhi ya “near-Arctic state” na kuwekeza katika tafiti na miradi ya kiuchumi inayohusiana na Greenland.
Katika kitabu ‘Geopolitics and Security in the Arctic’ ambacho ni mkusanyiko wa makala zilizoandikwa na Rolf Tamnes na Kristine Offerdal, waandishi wanaeleza kuwa mwelekeo huu umeilazimisha Jumuiya ya kujihami ya mataifa ya magharibi (Nato), chini ya uongozi wa Marekani, kuimarisha tahadhari yake ili kuzuia udhibiti wa kimkakati wa njia muhimu za Arctic.
Kwa upande mwingine, mabadiliko ya tabianchi yamekuwa upanga wenye makali mawili kwa Greenland. Kuyeyuka kwa barafu kunaleta changamoto kubwa za kimazingira na kijamii.
Hali hii inafungua fursa mpya za kiuchumi kupitia upatikanaji wa rasilimali za madini ya kimkakati.
Katika ripoti za kisayansi rasilimali hizi zinatajwa kuwa muhimu kwa teknolojia za kisasa kuanzia simu janja hadi nishati jadidifu.
Hali hii imeongeza hamu ya mataifa makubwa, hususan Marekani na China katika mustakabali wa Greenland.
Siasa za kisasa, mvutano wa 2025–2026
Katika uchaguzi wa Greenland wa mwaka 2025, suala la uhuru lilikuwa kitovu cha mjadala wa kisiasa. Wanasiasa waligawanyika kati ya kuharakisha safari ya kupata uhuru kamili na kuendelea na muundo wa sasa wa kujitawala ndani ya ufalme wa Denmark. Mjadala huu umevuka mipaka ya ndani na kuvutia umakini wa kimataifa. Kauli za viongozi wa Marekani kuhusu nia ya kuichukua Greenland zimeongeza joto la kisiasa, zikizua mjadala mpana kuhusu haki ya kujitawala na umiliki wa ardhi.
Kwa mujibu wa misingi ya sheria za kimataifa, mustakabali wa Greenland hauwezi kuamuliwa bila ridhaa ya watu wake. Greenland inakabiliwa na changamoto ya kihistoria: jinsi ya kusawazisha tamaa ya uhuru, mahitaji ya kiuchumi na shinikizo la kijiografia.
Ingawa ina rasilimali nyingi, utegemezi wa ruzuku kutoka Denmark bado ni suala nyeti. Wakati huohuo, uwapo wa kijeshi wa Marekani unaibua maswali kuhusu uhuru halisi wa maamuzi ya kisiasa.
Sasa Donald Trump ameibua mjadala wa kimataifa juu ya kusaka udhibiti wa Greenland kwa masilahi ya ulinzi wa kitaifa, akisema Marekani inahitaji kisiwa hicho ambako tayari ina kituo kikubwa cha kijeshi, ili kukabiliana na ushawishi wa Russia na China katika Arctic na kuongeza utayari wa kijeshi wa Marekani na Nato.
Kwa hotuba yake katika World Economic Forum ya 2026 huko Davos, Trump ametangaza nia yake ya kuitwaa Greenland na akasisitiza hatatumia nguvu za kijeshi, lengo likiwa kuongeza ushirikiano wa kipaumbele na washirika wa Nato kuhusu usalama wa Arctic.
Hata hivyo, kauli hii imeibua mjadala mkali kwani viongozi wa Greenland na Denmark wamekataa mara kwa mara wazo la kuachia kisiwa hicho, wakisisitiza kwamba: ‘Greenland si ya kuuza’ na mustakabali wake unapaswa kuamuliwa na watu wake wenyewe.
Ikiwa Marekani itaendelea kutilia mkazo suala hili kwa nguvu za kisiasa au kiuchumi, kuna hatari kuwa itasababisha mvutano mkubwa ndani ya Nato, hasa ikiwa Trump atajaribu kupitisha uamuzi wa kudhibiti kisiwa hicho bila ridhaa ya Denmark au ya kisiasa ya Greenland wenyewe.
Katika hali ya hatari zaidi, uvumi wa kutumia nguvu dhidi ya kiongozi wa kigeni utavunja msingi wa usalama wa pamoja wa Nato kanuni ya kuzishirikisha nchi wanachama wenzako badala ya kuzivunja na kuathiri imani ya washirika wa Marekani.
Kwa upande wa Greenland, shinikizo kama hili linaweza kusababisha hisia kali za kijamii, kama zilivyoonyeshwa na maandamano makubwa yaliyohubiri ‘Greenland si ya kuuza’ na kuongeza msukumo wa uhuru kamili, huku utegemezi wa kiuchumi na historia ya ulinzi ikibakia masuala ya msingi.
Kwa hiyo, mustakabali wa Greenland haujawahi kutegemea tu rasilimali zake na nafasi yake ya kimkakati, bali pia jinsi dunia itakavyoshughulikia nafasi yake ya haki ya kujitawala, uhusiano wa juu ndani ya Nato na sera ya ulinzi ya Marekani yenyewe.
Uamuzi wa kisiasa kuhusu iwapo Marekani ‘inapata’ kisiwa hicho unaweza kubadilisha si tu ramani ya usalama wa Arctic bali pia misingi ya sheria za kimataifa, ushirikiano wa kibiashara, na hata mahusiano ya muda mrefu kati ya nguvu za dunia.