BAADA ya kukosa ushindi katika michezo minne mfululizo, Tanzania Prisons itakuwa na kibarua kingine kizito itakapowakaribisha JKT Tanzania katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikipigwa katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Maafande hao hawajawa na matokeo mazuri kwani katika mechi nne za mwisho wamepoteza tatu na sare moja, huku mara ya mwisho kuonja pointi tatu ilikuwa Oktoba 21 walipoikanda Mbeya City mabao 2-1.
Baada ya mchezo huo, walipoteza dhidi ya TRA United 1-0, wakafa tena kwa Fountain Gate 1-0, kisha suluhu ya bila kufungana mbele ya Pamba Jiji na juzi wakalala bao 1-0 kwa Dodoma Jiji na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi saba.
JKT Tanzania imekuwa katika kiwango bora wikiwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 20 baada ya mechi 11 walizocheza, huku wakiwa hawajapoteza mchezo wowote kati ya mitano nyuma.
Katika dakika 450 walizocheza, wameshinda minne dhidi ya KMC bao 1-0 matokeo sawa na TRA United, wakaichapa Fountain Gate 2-0, suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar na kuizaba Singida Black Stars 1-0.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Zedekiah Otieno amesema mchezo huo ni muhimu kwao kurejesha matumaini na morali kwa wachezaji pamoja na mashabiki akiahidi kuwa liwake jua, inyeshe mvua lazima mpinzai wao aumie.
“Tunajua wapinzani namna walivyo msimu huu, tumekuwa na matokeo si mazuri sana, hivyo kesho (leo) tunahitaji kuanza upya ligi kupata ushindi ili kujiweka nafasi nzuri na kurejesha matumaini kikosini,” alisema Otieno.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema kila mchezo kwao ni vita ya pointi tatu na kwamba wanafahamu ugumu wa mechi hiyo, lakini hesabu zao ni kuendelea kufanya vizuri.
“Vijana wanapambana na malengo yetu ni kushinda kila mchezo, tunafahamu ugumu na umuhimu wa mchezo wa kesho, tunachohitaji ni nidhamu uwanjani kuwaheshimu wapinzani na kufanya wajibu wetu,” alisema kocha huyo.