Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema kumuenzi mwasisi wa chama hicho, hayati Edwin Mtei (94), kunapaswa kuambatana na dhamira ya dhati ya Taifa ya kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Amesisitiza kuwa hilo lilikuwa miongoni mwa maono ya msingi ya waasisi wa chama hicho akiwamo Mtei katika kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria nchini.
Mnyika ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Januari 24, 2026, wakati wa kumbukizi ya maisha ya Mzee Mtei zilizofanyika Arusha, kabla ya maziko yake yaliyopangwa kufanyika mchana wa leo nyumbani kwake Tengeru.
Akizungumza mbele ya wanafamilia, wanachama wa Chadema, wadau wa demokrasia na viongozi wengine mbalimbali, Mnyika amesema ni wajibu wa Wanachadema na Watanzania wote wanaoguswa na masuala ya demokrasia kushirikiana katika kutimiza maono ya Mtei, aliyekuwa pia Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nawaomba Wanachadema na Watanzania wote wanaoguswa na demokrasia nchini. Kuna mambo mawili muhimu ambayo naamini ni sehemu ya kumuenzi Mzee Mtei.
“Kwanza, wazee walipoasisi mageuzi na kuanzisha Chadema walikuwa na wazo la Katiba Mpya. Wakati umefika wa kuyatekeleza maono hayo kwa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya nchini,” amesema Mnyika.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche (kulia) akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Suzan Lyimo (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika wakati wa ibada ya maziko ya Mwasisi wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei nyumbani kwake Tengeru, wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha leo Jumamosi Januari 24,2026. Picha na Filbert Rweyemamu
Ameongeza kuwa jambo la pili katika kumuenzi Mtei ni kuendeleza mapambano ya kidemokrasia ili kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanapatikana kupitia ushindani wa vyama vingi.
“Tanzania imetawaliwa na chama kimoja tangu uhuru. Mzee Mtei alikuwa na maono ya kuona chama kingine kikishika dola. Tuendelee kushirikiana ili siku moja Chadema ishike dola na kuongoza Serikali,” amesema.
Mnyika amemwelezea Mtei kama kiongozi mwenye misimamo thabiti, maadili ya hali ya juu na aliyeheshimu kwa dhati misingi ya demokrasia, akisisitiza kuwa urithi wake utaendelea kuishi ndani ya Chadema na nje ya chama hicho.
Akitoa mfano wa msimamo huo, Mnyika amesema kati ya mwaka 2003 na 2006 kulikuwa na mjadala mkubwa ndani ya Chadema kuhusu mabadiliko ya bendera ya chama, ikiwemo mapendekezo ya kuondoa alama ya vidole viwili na badala yake kuweka alama ya ngumi.
“Mzee Mtei alisema mnaweza kubadili vitu vingine vyote, lakini alama ya vidole viwili isiondolewe. Alama hiyo ndiyo roho ya chama. Mpaka leo imeendelea kubaki,” amesema.
Aidha, Mnyika amesema Chadema tangu mwaka 2021 ilianza mazungumzo ya ndani kuhusu namna bora ya kumuenzi Mtei, ambapo mapendekezo mbalimbali yalitolewa ikiwemo kuanzishwa kwa taasisi maalumu ya kumbukumbu yake.
Ameeleza kuwa vikao vya kikatiba vya chama vitakavyoendelea vitafanya uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo jengo au ukumbi maalumu utaitwa jina la Mzee Mtei, kama sehemu ya kuenzi mchango wake katika historia ya siasa za Tanzania.
Kumbukizi hizo zimewakutanisha viongozi wa chama hicho, wanachama, wanaharakati wa demokrasia na wananchi waliotaka kutoa heshima zao za mwisho kwa mmoja wa waasisi wa siasa za mageuzi nchini.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, amesema nyumba ya Mtei ilikuwa kimbilio muhimu la upatanishi wa kisiasa na kijamii, akimtaja kama mpatanishi wa kipekee aliyetoa mchango mkubwa katika historia ya chama hicho na taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika kumbukizi hiyo, Golugwa amesema misingi na falsafa aliyoiasisi Mtei, hususan kauli mbiu ya “hakuna kulala mpaka kieleweke”, imeendelea kuwa mwanga na dira kwa viongozi wa Chadema waliopo madarakani ndani ya chama hicho.
“Hakuna kulala mpaka kieleweke ndilo neno ambalo aliliasisi Mzee Mtei. Mara nyingi ukija nyumbani kwake, lazima aseme neno hilo. Nyumba hii ilikuwa ni kimbilio; alikuwa mpatanishi wa kipekee sana,” amesema Golugwa.
Ameeleza kuwa viongozi wa sasa wa Chadema wamepokea kijiti cha uongozi kwa ujasiri mkubwa, wakiahidi kuendeleza misingi ya haki, uwajibikaji na mapambano ya kidemokrasia aliyoyaacha Mtei.
Golugwa amesema urithi wa fikra na msimamo wa Mtei haukuwa wa chama pekee, bali ulikuwa kwa masilahi mapana ya taifa, akisisitiza kuwa Chadema itaendelea kusimamia misingi hiyo bila kuyumba.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Ruth Mollel, amesema mwasisi huyo ameacha alama ya ujasiri na uthabiti.
Alitolea mfano namna Mtei akiwa Waziri wa Fedha na Mipango, alitofautiana na Rais Mwalimu Nyerere (hayati), katika sera za fedha na kujiuzulu wadhifa huo.
“Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya baba yetu kwa jinsi alivyokidumisha hiki chama mpaka sasa hivi tuna chama kikubwa na imara sana.
“Ametuachia ‘legacy’ (alama) ya ujasiri na uthabiti kama mtakumbuka alitofautiana na Mwalimu Nyerere na akajiuzulu ni kwa sababu ya misimamo yake na sisi tutaendeleza kusimamia tunachokiamini kwa uthabiti bila kuogopa,” amesema.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel, amesema watamuenzi mwasisi huyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha chama hicho kinaendelea katika kupigania mageuzi ya kweli.
“Uwepo wa Mzee Mtei Chadema unathibitisha siyo chama cha watu wa kawaida ni chama makini na katika kupigania mageuzi ya kweli, siasa za mageuzi watu wengi wameyumba kwa kukosa uhuru wa kiuchumi,” amesema.
Mwenyekiti wa baraza la Wazee, Suzan Lymo, amesema mwasisi huyo alikuwa msitahimilivu hakuwa mbinafsi hivyo kuwaomba vijana waache usaliti.
“Maisha ya binadamu ni hadithi tu inategemea hadhithi hiyo unaiwekaje, hadhiti yake itasomwa vizuri amefanya mambo makubwa katika nchi hii ameasisi sera nyingi za fedha.
“Alikuwa mstahimilivu hakuwa mbinafsi kwa vijana wa sasa tunawaomba sana tuache usaliti mzee angekuwa msaliti Chadema isingekuwa hapa tushikamane tulete mageuzi katika nchi yetu,” amesema.
Rafiki wa Chadema, Jenerali Ulimwengu amesema Mzee Mtei kati ya vitu ambavyo hakuvipenda ni pamoja na ‘uswahili’, alioutafsiri kama kuahidi mambo yasiyotekelezeka.
“Uswahili ni jambo baya sana na alisema maana ya uswahili ni kusema kitu ambacho unajua si kweli na unatarajia unayemwambia ataamini ni kweli, uswahili ni kutoa ahadi uanzojua hutazitekeleza.
“Uswahili ni upangaji wa maneno mengi ambayo ndani yake hamna kitu, uswahili naongeza mimi ni kuahidi mambo ambayo katika dhamira yako huna nia ya kuyatekeleza na uswahili ni ugonjwa mbaya sana unatufanya tushindwe tuketekeleza tuliyokubaliana.”
Mtei alizaliwa Julai 12,1932 Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro na alishikilia nyadhifa mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa BoT, mwaka 1966 na miaka 12 baadaye akaja kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ambapo alitumikia nafasi hiyo kuanzia 1978 hadi 1981 alipojiuzulu.
Novemba 1982 aliteuliwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF),Mwenyekiti Mwanzilishi wa Tanzania Coffee Research Insitute (TaCRI) kuanzia mwaka 2001 hadi 2008.